KIKOSI cha Simba, usiku wa kuamkia jana Jumamosi, kilifanikiwa kutua salama katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Sir Seretse Khama nchini Botswana, kabla ya leo Jumapili kuwakabili Jwaneng Galaxy katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza.
Simba imeondoka na kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mchezo huo unaotarajia kupigwa leo Jumapili
kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana, jijini Gaborone kuanzia saa 10:00 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Spoti Xtra limezipata kutoka nchini humo, zinasema kuwa timu hiyo
ilifika saa nane usiku ambapo ilitumia muda wa saa moja kukamilisha taratibu za uhamiaji, kabla ya kutoka na kuelekea Hoteli ya Avani ambayo ina hadhi ya nyota nne.
Mtoa taarifa ambaye ameambatana na timu hiyo, alienda mbali kwa kusema tayari wenyeji wao wameshaingiwa na mchecheto.
“Unajua tayari tulishatanguliza watu wetu ambao walikuja kuweka mambo sawa kwa siku kadhaa wakiwa hapa Gaborone wakawa kama wameuteka mji kwa kujua kila kitu na wapi timu ifikie.
“Hivyo tuna uhakika wa kupata matokeo mazuri kwa kuwa tupo kwenye mazingira salama hali ambayo imewapa hofu wapinzani kuelekea kwenye mchezo wetu wa kesho (leo) Jumapili,” alisema mtoa taarifa.