SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema alikuwa na ndoto ya kuwa hakimu kama alivyokuwa baba yake mzazi lakini Mkuu wake wa Shule (Headmaster) alimpangia kuelekea kwenye mchepuo wa sayansi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM) ametoa kauli hiyo leo tarehe 7 Oktoba, 2021 wakati akihutubia katika uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa mkoani Dodoma.
Amesema wakati huo akiwa kidato cha tatu katika Sekondari ya Kibaha alimfuata mkuu wake wa shule na kumwomba ampangie mchepuo wa sanaa lakini alimfukuza ofisi kwake kisha akampangia mchepuo wa sayansi.
“Baba alikuwa hakimu kule Mlali, Sagara, Kongwa, Mpwapwa hadi Ukerewe yaani alikuwa anahamishwa sana, nilikuwa na passion (hamu) siku moja niwe hakimu wa mahakama ya mwanzo sikufikiria kuwa jaji. Mungu hakujalia lakini nayo ni maisha sasa nimekuwa mtunga sheria sio mtafsiri sheria,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa Wana-Kibaigwa kufaidika na mahakama hiyo kwa kupinga ukatili wa kijinsia.
“Wa kwanza ambao mnatakiwa mfaidike na huduma hii ni akina mama, yaani ukipigwa kofi break ya kwanza ni hapa, wanaume acheni ukatili wa kijinsia ili mahakama isije kuanza na nyie.
“Na wale wanawake wanaowaonea wanaume mahakama hii hapa. Baadhi ya wanaume wanafinywa wananyamaza tu, sasa mahakama imekuja tuje tupate ukombozi hapa,” amesema.
Ndugai amesema Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma amemkata ngebe baada ya kukamilisha ujenzi wa jengo la mahakama ya mwanzo Kibaigwa mkoani Dodoma kwa kuwa kila alipokuwa akikutana naye alikuwa akimkumbushia mahakama hiyo.
Aidha, akizungumza katika uzinduzi huo, Jaji mkuu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amegiza uongozi wa mahakama mkoani Dodoma kuhakikisha mahakama hiyo yenye jengo la kisasa kutumika vema kwa kuweka mifumo yote ya kiteknolojia ili kurahisisha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.
Amesema kwa kuwa kata hiyo ya Kibaigwa ambayo ni mji mdogo, unaelekea kukua kwa kasi kutokana na shughuli nyingi za kibiashara, hivyo wananchi wanapaswa kulitunza jengo hilo lililojengwa kwa thamani ya zaidi ya Sh milioni 797 kwa kuwa ni mojawapo ya kivutio katika mji huo.