USHUJAA ulioonyeshwa na mlinda mlango wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Aishi Manula, huku winga Simon Msuva akitekeleza majukumu yake vema ya kuliona lango la Benin kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022, liliifanya Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 jana.
Winga wa Taifa Stars, Simon Msuva, akiwatoka mabeki wa Benin kabla ya kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni na kuifanya Tanzania kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar iliyopigwa Uwanja wa L'Amitie, Cotonou, Benin jana. MPIGAPICHA WETU
Bao la dakika ya sita lililofungwa na winga wa kimataifa wa Tanzania anayeichezea Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, Msuva, ndilo lililowafanya Wabenin hao jana kulazimika kulala mapema tu baada ya mchezo huo uliopigwa Uwanja wa L'Amitie, Cotonou nchini Benin.
Stars imelipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 nyumbani, Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, hivyo kupindua meza ugenini kibabe.
Katika mchezo huo Stars ilikuwa nyuma ya mpira kwa muda mrefu, huku kipa Manula akiibuka shujaa kwa kuokoa michomo na hatari nyingi kutoka kwa wachezaji wa Benin.
Ulikuwa ni mpira wa kurushwa na Israel Mwenda pembeni mwa uwanja alimrushia Msuva, ambaye aligeuka na kuanza kuwalamba chenga mabeki wawili wa Benin, kabla ya kuachia shuti kali lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni, lililomwacha kipa Saturnin Aliagbe akiwa hana la kufanya.
Baada ya bao hilo la mapema, Stars ilionekana kurudi nyuma na kuanza kujilinda, mbele ikimwacha Kibu Denis na wakati mwingine akisaidiana na nahodha Mbwana Samatta.
Manula aliiweka salama Stars dakika mbili kabla ya mapumziko, baada ya Djallilou Ouorou kupenyezewa pasi safi ndani ya eneo la hatari, na kupiga shuti kali ambalo aliliokoa kwa mguu wa kushoto, kabla ya mpira huo kufagiliwa mbali na Bakari Mwamnyeto.
Kipindi cha pili, Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen alifanya mabadiliko, akiwatoa Kibu, Feisal Salum, Msuva na kuwaingiza, Ralients Lusajo, Zawadi Mauya, na Abdul Selemani, ambaye naye baadaye alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Edward Manyama.
Chabel Gomes, nusura aisawazishie Benin bao dakika ya 53, alipiga kichwa mpira wa krosi, lakini Manula alichupa na kuudaka kwa ustadi wa hali ya juu.
Mchezaji hatari aliyeisumbua ngome ya Stars kwenye mechi ya kwanza Dar es Salaam, Michael Pote, ambaye hata kwenye mchezo wa jana alionekana kufurukuta, aliingia ndani ya eneo la hatari na kuachia shuti kali, lililookolewa na Manula dakika ya 59.
Dakika nne baadaye krosi ya Steve Mounie aliyefunga bao pekee nchini, ilikuwa ikisubiriwa na wachezaji wawili wa Benin, David Kiki na Mateo Ahlinvi waliielekeza wavuni, lakini kipa huyo aliruka na kuudaka kwenye miguu ya wachezaji hao ambao, wakiishia kuingia nyavuni, mpira ukibaki salama mikononi mwa Manula.