Marekani imekubali kutoa misaada ya kiutu kwa Waafghanistan wanaokabiliwa na mzozo wa kiuchumi ingawa imekataa kuitambua kisiasa serikali ya Taliban inayotawala taifa hilo kwa sasa.
Taarifa hii imetolewa mwishoni mwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya mahasimu hao wa zamani tangu kukamilika kwa mchakato wa Marekani wa kuwaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan uliogubikwa na ghasia mwishoni mwa mwezi Agosti.
Marekani kwenye taarifa yake imesema kwa kifupi kwamba pande hizo mbili zilijadiliana kuhusiana na msaada huo wa kiutu ambao imekubali kuutoa moja kwa moja kwa watu wa Afghanistan ingawa imesema hayafungui njia ya kuitambua serikali ya Taliban.
Mazungumzo hayo yalifanyika Doha huku Taliban ikisema yalikwenda vizuri na Marekani ikisema yalikuwa ya uwazi na ya kitaalamu.