TANROADS yang'ara Tuzo za Taasisi bora za Serikali




Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imeng’ara katika tuzo za taasisi bora za serikali kwa uwezeshaji wananchi kiuchumi baada ya kuwa mshindi wa kwanza na kutunukiwa tuzo na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

TANROADS ilitunukiwa tuzo hiyo Jumatatu, Oktoba 4, 2021 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa katika Kongamano la tano la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, lililofanyika jijini Dodoma.

Tuzo hizo hutolewa na NEEC katika kila kongamano la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, zikihusisha makundi mbalimbali yanayoshindania ambapo kwa mwaka huu, yalikuwepo makundi saba.

TANROADS ilishindania tuzo hiyo katika kundi la Taasisi za serikali, lililohusisha taasisi mbalimbali na kuibuka mshindi wa kwanza huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Mamlakaya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Utaratibu wa upatikanaji wa mshindi wa tuzo hiyo, kwa mwaka huu, ulihusisha uundwaji wa kamati ya kujitegemea iliyokuwa na wajumbe wanne kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na TAMISEMI.

Vigezo vinavyohusishwa kushindania tuzo hizo ni kila mshindi anapaswa kupata alama zisizopungua 50 na katika kila kundi hupatikana mshindi wa kwanza, wa pili na mshindiwa tatu.

Kila kundi huwa na washindani watano na ushindani hufanyika kwa kuzingatia vigezo.

Makundi yaliyokuwepo katika tuzo za mwaka huu ni kundi la Mikoa, Wizara, Taasisi za Serikali, Mifuko ya Kijamii, Programu za uwezeshaji, taasisi zilizoshirikiana kutekeleza programu za Baraza, Wajasiriamali na Asasi za kiraia.

TANROADS imekuwa taasisi ya mfano kwa uwezeshaji wananchi kiuchumi kutokana na umahiri katika utekelezaji wa majukumu yake, yakiwemo ya ujenzi wa barabarazinazounganisha Mikoa ambapo miradi inayotekelezwa imeleta faida nyingi za kiuchumi, kijamii na kibiashara kwa wananchi.

Serikali baada ya kuridhika na ufanisi wa TANROADS iliongeza jukumu la ujenzi wa viwanja vya ndege, hatua ambayo imefikiwa baada ya serikali kuamini ufanisi mkubwa wa TANROADS katika miradi ya ujenzi wa Barabara na Madaraja nchini.

Kuongezwa kwa jukumu hilo, ni kielelezo halisi cha utendaji bora na ufanisi wa TANROADS katika kazi ambazo kimsingi zinabeba dhima ya kuhudumia wananchi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad