Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema, bado Tanzania inakabiliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu hapa nchini hasa katika maeneo ya uhuru wa habari na vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Oktoba 5, 2021 na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa wakati wa Mkutano wa mapitio ya hali ya haki za binadamu uliyoandaliwa na mtandao huo na kukutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo.
Olengurumwa amesema ripoti yao inaonesha kuwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2017 hadi 2020 kumekuwa na ukiukwaji huo licha ya Serikali kukubali baadhi ya mapendekezo 133 yaliyotolewa na watetezi wa haki za binadamu.
Amesema Kukosekana kwa uhuru wa kujieleza, utungwaji wa sheria kali kwa vyombo vya habari, kuzuiwa kwa watetezi wa haki za binadamu kutekeleza majukumu yao, vyote hivyo vimesababisha kuzolotesha haki za binadamu nchini.
“Yapo maeneo ambayo nchi imefanya vizuri karibia asilimia 60, lakini bado tunaona ukiukwaji wa haki za binadamu unaendelea kutokea kwani uhuru wa habari unaendelea kupungua, watetezi wanapata shida katika ufanyaji kazi kwa miaka hiyo minne, hivyo tunaamini kupitia mikutano hii tutatoka na mapendekezo mengine ambayo yatafanyiwa kazi na serikali,” amesema
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju amesema Serikali imekuwa ikithamini mchango wa asasi za kiraia na kuheshimu haki za binadamu.