Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha miezi sita tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani, hatua mbalimbali zimepigwa ikiwemo uchumi kuongezeka.
Ameeleza hayo leo Jumapili Oktoba 10, 2021 wakati akizinduzi Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
''Kwenye robo ya pili ya mwaka huu, kutoka Aprili hadi Juni, uchumi umeongezeka hadi kufikia asimilia 4.3 ukilinganisha asilimia 4 katika kipindi hicho mwaka uliopita,'' ameeleza Rais Samia.
Aidha, ameongeza kuwa, ''Hadi mwezi Agosti 2021, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani Bilioni 5.8 iliyotosheleza kuagiza bidhaa na huduma za nje kwa kipindi cha miezi 6 ikilinganishwa na dola bilioni 4.9 mwaka uliopita”.