Ujenzi daraja la JPM wadaiwa kuhujumiwa




MADAI kuhusu kuhujumiwa kwa daraja la JPM linalojengwa eneo la Kigongo-Busisi, mkoani hapo kwa gharama ya Sh. bilioni 700 yameibuliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza, Katibu Mwenezi wa CCM katika Wilaya ya Ilemela, Denis Nyamlekela alisema, Oktoba 14, mwaka huu, walipata taarifa mbaya kutoka kwa mmoja wa mafundi wa mradi huo kwamba vipimo vya bomba na nondo zilizokubaliwa katika mkataba vimechakachuliwa.

Alisema mtoa taarifa huyo ambaye mpaka sasa anafanya kazi katika mradi huo, alisema vipimo vya mabomba na nondo zilizokubaliwa katika mkataba wa ujenzi uliosainiwa vimechakachuliwa.

Nyamlekela alisema Oktoba 14, mwaka huu yeye na kamati ya siasa wakitokea wilayani Chato walipata taarifa hiyo na kwamba vipimo vya mabomba yanayoshuka chini majini vimechakachuliwa na kwamba kuna hatari ya daraja hilo kutokuwa imara.

Mjumbe huyo wa kikao hicho alisema, kuna haja ya kufanya uchunguzi kuhusu taarifa hiyo ili kujiridhisha ukweli wake.


 
Aliongeza kuwa mradi huo ni muhimu kwa uchumi wa nchi na umegharimu fedha nyingi ni lazima tahadhari zote zichukuliwe ili kuulinda.

Daraja hilo ambalo linajengwa na kampuni kutoka nchini China, linaunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema.

Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Mwanza, Antony Diallo, alisema kuna haja ya kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo.


Hata hivyo, Diallo alionyesha wasiwasi wake kuhusu ukweli wa taarifa hizo kwa madai kuwa mradi huo unasimamiwa na wataalamu walioaminiwa na serikali.

"Mimi siamini taarifa hizi kwamba vipimo vya bomba na nondo vilivyokubaliwa kitaalamu katika mkataba kwa sasa havifuatwi, ila uchunguzi ufanyike," alisema Diallo ambaye alisimamia kikao hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, alipouliza kuhusu madai hayo alisema, haamini kama ni kweli.

Alisema hawezi kuamini taarifa za barabarani, lakini alisema uchunguzi utafanyika ili kujiridhisha kuhusu madai yaliyotolewa.


 
Aliongeza kuwa kuna wataalamu wa kutosha walioaminiwa kusimamia mradi huo mkubwa na kimkakati mkoani mwake.

Kikao hicho ambacho pia kilihusisha watendaji, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa na Watendaji wa serikali mkoani Mwanza kilikuwa kwa ajili ya kupokea utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad