MARA baada ya kuwepo taarifa za baadhi ya watu kuuza kiharamia albam ya Mfalme wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba au King Kiba ya Only One King mtaani, Serikali kupitia Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imetoa onyo ikikemea vikali hilo na kusisitiza kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Alhamisi na Ofisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa COSOTA, Doreen Anthony Sinare, watakaokamatwa wakiuza albam hiyo ya Kiba itakuwa imekula kwao kwani adhabu iliyoainishwa na sheria ni shilingi milioni 20 au kwenda jela miaka mitano.
“Hivi karibuni baada ya mmiliki wa Lebo ya Kings Music na msanii wa muziki, Ali Kiba kutoa taarifa ya kupatikana kwa albam yake ya Only One King katika majukwaa mbalimbali ya mtandaoni ya kusambaza muziki (digital platform), kumeibuka watu wanaodurufu na kuuza mitaani pasipo makubaliano yoyote na yeye hii ni kosa kisheria,” anasema Sinare na kuongeza;
“Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7 ya mwaka 1999 imeeleza kuwa kusambaza kazi ya mbunifu yeyote bila ridhaa yake ni kosa kisheria na adhabu yake ni faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo cha miaka mitatu mpaka mitano au vyote kwa pamoja,” imeeleza taarifa hiyo.
Albam hiyo ya Kiba iliingia sokoni Ijumaa ya wiki iliyopita ikiwa na nyimbo 16 ambazo amewashirikisha wasanii zaidi ya 10 kutoka Tanzania, Kenya, Nigeria, Afrika Kusini na Ghana. Hii ni albam ya tatu kwa mwimbaji huyo baada ya Cinderella (2007) na Ali K4Real (2009).