Unaambiwa Harmo Amfanyia Umafia Mondi Marekani





KIBAO kimegeuka! Ndivyo wasemavyo wananzengo baada ya msanii wa muziki nchini Tanzania, Abdul Rajab au Harmonize kudaiwa kumfanyia umafia aliyekuwa baba yake mlezi kimuziki, Nasibu Abdul au Diamond Platnumz, Gazeti la IJUMAA limeng’atwa sikio.


Harmonize au Konde Boy Mjeshi ametajwa kuwa ndiye msanii pekee wa Kitanzania aliyechaguliwa kufanya shoo katika tamasha kubwa duniani la Interswitch One Africa Music Fest 2021 linalofanyika jijini New York nchini Marekani Oktoba Mosi, mwaka huu; nafasi ambayo kwa miaka mingine huchukuliwa na Diamond au Mondi.


Harmonize au Harmo anayetikisa na ngoma yake ya Teacher, sasa ataonesha uwezo wake mbele ya mastaa kutoka nchi mbalimbali za duniani wakiwemo Mr Flavour, Olamide, Tiwa Savege, Oclade, Bella Shmurda, Wurld, Rema na Tome; wote kutoka nchini Nigeria.


Wengine ni; Kranium kutoka Jamaica, Busiswa kutoka Afrika Kusini, Kwaw Kese kutoka Ghana na D12 wa Marekani.

Ikumbukwe kwamba, Harmo alipata umaarufu katika soko la muziki baada ya kujiunga na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya C.E.O wake, Diamond; ilikuwa mwaka 2015.


Mwaka 2020, Konde Boy aliachia album yake ya Afro East ambayo ilifanya vizuri ndani na nje ya Tanzania huku akiwa amewashirikisha mastaa wakubwa kutoka nje ya Bongo kama Burna Boy, Khaligraph Jones, Mr Eazi na wengine wengi.


Konde Boy Mjeshi mwenye umri wa miaka 31 hivi sasa, anamiliki lebo kubwa ya muziki Afrika Mashariki ya Konde Music World Wide ambayo inasimamia vipaji vya wasanii sita; Killy, Ibraah , Anjella, Country Wizzy, Cheed na Skales wa Nigeria kwa upande wa Afrika Mashariki.


TAMASHA LA ONE AFRICA MUSIC

Tamasha hilo ni miongoni mwa matamasha makubwa ya muziki duniani, kwani hutoa nafasi kwa wanamuziki kutoka nchi mbalimbali kupafomu sehemu moja na kuonekana kila kona ya dunia.


Hadi sasa, tamasha hilo linashikilia rekodi ya kualika wasanii wakubwa kwa ajili ya kutumbuiza kama Wizkid, Davido, Diamond, King Kiba, Casper Nyovest, Phyno na wengine kibao ambao wakishaonekana kwenye jukwaa hilo, basi hutambulika kama wasanii wakubwa.


Kama ulikuwa hujui, tamasha hili kwa mwaka huu linafanyika New York nchini Marekani katika ukumbi mkubwa wa Coney Island Amphitheater. Ukumbi huu ulianza kutumika rasmi Julai, 2016 huku ukiwa na uwezo wa kuingiza zaidi ya watu elfu tano waliokaa kwenye viti na wachache katika sehemu ya kusimama.


Tiketi ziliuzwa kwa bei tofauti kulingana na eneo mtu atakalokaa; tiketi moja ilianzia shilingi elfu 70 hadi laki tano.


HARMONIZE KUTOKA CHITOHOLI HADI MAREKANI

Harmo ametoka mbali mno, unaweza kufikiria umbali uliopo kutoka katika Kijiji cha Chitoholi, Tandahimba mkoani Mtwara hadi Dar kisha New York nchini Marekani. Konde Boy amepambana!


Kwa mtu wa kawaida tu kule kijijini akikuambia ana ndoto za kufika Marekani, unaweza kumuona kichaa au anaota ndoto ya mchana.

 

Akiwa ametokea katika familia duni ya kijijini huku akiwa na wazazi walioshika Dini ya Kiislam, Harmonize alianza harakati zake za kimuziki akishambuliwa na baba yake ambaye alihitaji asome elimu ya dunia na ya dini na aachane na muziki.

 

Harmo aliachana na shule na kujikita katika muziki ambao haukuwa unamlipa kwa kipindi cha nyuma huku akifanya biashara ndogondogo kama kuuza maji na matunda katika Mitaa ya Kariakoojijini Dar hivyo ni machinga halisi ili mkono uwende kinywani na kupata pesa za kuusukuma muziki wake.

 

HARMONIZE AWAKALISHA WAKUBWA

Kwa mara ya kwanza, Konde Boy Mjeshi alionekana katika tamasha la kuibua vipaji la BSS ambapo baada ya kutumbuiza aliambiwa na majaji kuwa hawezi kuimba na atafute shuhuli nyingine za kufanya, lakini kimoyomoyo aliipinga sauti ile.

 

Baadaye alikutana na Diamond kwa mbinde mno katika Ukumbi wa Dar Live pale Mbagala jijini Dar na hapo ndipo ukawa mwanzo wa maisha mapya ya ustaa.

Harmo amekuwa msanii pekee wa Tanzania kwa mwaka 2021 kuchaguliwa kwa kura kati ya mastaa kibao Bongo, kupafomu katika tamasha hilo.

 

Mara ya mwisho Diamond kuchaguliwa kupafomu katika tamasha hilo ni mwaka 2019 ambapo Harmonize naye alishiriki kule Dubai.

Kwa miaka ya nyuma Diamond au Simba alikuwa akichaguliwa yeye kutoka Tanzania kwa ajili ya kupafomu katika tamasha hilo, hii ni kutokana na ukubwa alionao katika soko la muziki duniani.

 

Ila kwa sasa, Harmonize amekuwa akichaguliwa mfululizo, huku wananzengo wakihusianisha na uwezo aliokuwa nao Mondi zamani na namna Harmo anavyochaguliwa kushiriki katika tamasha hilo kwa sasa, huwenda uwezo na ukubwa wa Mondi sasa upo kwa Konde Boy Mjeshi!

 

Kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, Harmo ametajwa kutumbuiza katika tamasha hilo huku akimpiga chini Mondi ambaye ndiye alikuwa kinara kwa Tanzania kuitwa kupafomu miaka ya nyuma.

 

ZIARA YA HARMONIZE MAREKANI YATAJWA

Baadhi ya vyanzo vinadai kuwa, huwenda kuna umafia ambao umefanywa na Harmonize ambaye yupo nchini Marekani kwa ajili ya ziara za shoo zake hivyo inawezekana huko ndiko alikoonekana na kupewa shavu hilo.

 

NENO LA MENEJA MJERUMANI

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA juu ya mafanikio ya Harmonize wakati huu wakiwa nchini Marekani, meneja wa msanii huyo, Beauty Mmary almaarufu Mjerumani anasema kuwa, ni dalili njema kwamba muziki wa Bongo umependa.

 

“Ni ishara kwamba muziki wetu unasikilizwa kwenye mataifa tofautitofauti, kwa hiyo muziki umefika mbali na tunashukuru kwa namna tunavyopokelewa hapa Marekani, lengo letu ni kuona muziki unafika mbali na fursa tunayopata tunashukuru kwa sababu zinamsogeza Harmonize kwenye malengo ambayo anataka kuyafikia,” anasema Mjerumani na kuongeza;

 

“Tunaamini kwamba tunachokifanya ni kwa manufaa ya industry nzima ya muziki wa Tanzania na siyo kwa Konde Gang au Harmonize pekee.

 

“Ushindani wa ndani si mbaya kwa sababu unatukuza, lakini tunapotoka nje ushindani si wa sisi kwa sisi ni sisi dhidi ya mataifa mengine, kwa hiyo lengo letu liwe ni kuwa na wasanii wengi wa kimataifa kama walivyo wengine kutoka mataifa mengine ambao ni wengi.”

STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad