Hifadhi ya Taifa ya Mikumi licha ya kusifika kuwa na wanyama wengi kumekuwa na utalii wa kutembea kwa miguu (Walking) ambapo inamsaidia mtalii kuona na kujifunza mambo mengi kwa uhalisia.
Akizungumza katika hifadhi hiyo Afisa Mhifadhi Msaidizi Bw.Allan Mushi amesema kuna umuhimu wa watalii kutalii kwa kutembea kwa miguu katika hifadhi kwani ni rahisi kwake kutambua na kuona mambo mengi yaliyopo kwenye hifadhi.
“Ukiwa unafanya utalii wa kutembea kwa miguu kuna vitu vingi vya kujjifunza mfano, kuna nyao za wanyama, kinyesi cha wanyama na hata muda mwingine kutambua tabia za wanyama”. Amesema Bw.Mushi.
Aidha Bw.Mushi amesema kuna muda unaweza ukatambua muda ambao wanyama wamepita katika eneo fulani kwa kutazama unyayo wa miguu pamoja na kinyesi cha mnyama katika eneo fulani.
Amesema kabla ya zoezi la kutalii kwa kutembea kwa miguu hutoa elimu kwanza kwa watalii pindi kukitokea kwa mnyama mkali mbele yao wawezee kufanya nini ili asiweze kudhurika.
Pamoja na hayo Bw.Mushi amesema katika zoezi la kutalii kwa kutembea kwa miguu usalama huwa upo kwani lazima kuwepo kwa askari wenye silaha wakiwaongoza watalii katika maeneo ambayo kuna wanyama.