VITA kubwa ya namba imeibuka kwenye kikosi cha Yanga baada ya wachezaji ambao walikuwa nje kwa majeraha kurejea na wengine kuonyesha uwezo mkubwa kwenye mazoezi.
Vita kubwa ipo kwenye nafasi ya beki ya kushoto ambayo msimu uliopita ilikuwa inamilikiwa na Yassin Mustapha, kwa bahati mbaya akaumia na Adeyum Saleh kurithi mikoba.
Dirisha lilipofunguliwa Yanga ikamsajili Bryson Raphael kutoka KMC, naye hajaonekana kwenye timu hiyo kwa kuwa alisajiliwa akiwa na majeruhi.
Sasa taarifa kutoka kambi ya Yanga ambazo Championi Jumatatu zimepata ni kwamba wachezaji wote hawa wamepona na wameanza mazoezi na wanapambana kwa nguvu mazoezini kuweza kurudi kundini.
Ubaya kwa wachezaji hao ni kwamba beki ya kushoto ipo chini ya Shomari Kibwana, ambaye amekuwa akiitendea haki na kuna kibarua kingine cha kumweka nje.
Balama Mapinduzi naye ameanza matizi na anakwenda kutishia nafasi ya Farid Mussa, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke na Yacouba Sogne ambao nao hawana makazi ya kudumu kwenye eneo la kiungo.
Kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze alisema: “Kwa sasa Yanga inawahitaji wachezaji wote kuwa timamu kiafya kwa sababu wana kazi kubwa iliyopo mbeleni, ushindani ukiongezeka kwenye kikosi ndiyo mwanzo wa kupata timu bora.”
Hii inaonyesha kuwa pasua kichwa tena kwa kocha wa Yanga Nasredinne Nabi ambaye wikiendi ijayo anakwenda kucheza mchezo wake wa tatu wa Ligi Kuu Bara.
ISSA LIPONDA, Dar es Salaam