Dar es Salaam. Mkutano wa kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi na wadau wa siasa nchini uliopangwa kufanyika kesho, umeahirishwa kwa kile kinachodaiwa ni kutoa nafasi kwa wadau wengi zaidi kushiriki kikamilifu.
Kabla ya kuahirishwa kwa mkutano huo, vyama vya Chadema na NCCR Mageuzi vilishatangaza kutoshiriki huku vikitoa masharti kwa Ofisi ya Msajili.
Mkutano huo ambao sasa unatarajiwa kufanyika Desemba kwa tarehe itakayotangazwa baadaye na utahusisha wadau tofauti wakiwamo wa vyama vya siasa vilivyotangaza kuususia kwa sababu tofauti.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib alisema mkutano huo hautakuwepo kesho kama ulivyopangwa awali, lakini maandalizi yanaendelea kwa kuwa utafanyika mwezi Desemba, mwaka huu.
Alisema wadau wote wameshajulishwa kuhusu kuahirishwa kwa mkutano huo uliotarajiwa kuleta suluhu ya sintofahamu ya kisiasa nchini, hasa mvutano kati ya vyama vya siasa na Jeshi la Polisi.
Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia kuhusu kuahirishwa kwa mkutano huo, Msajili wa vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi aliomba atafutwe leo ofisini kwake kwamba ndio atakuwa na nafasi ya kuzungumzia suala hilo.
Septemba 20, Jaji Mutungi alitoa taarifa ya nia ya kufanyika kwa mkutano huo ukitanguliwa na mikutano mingine ya maandalizi ambayo tayari ilishafanyika na ulikuwa umebaki mkutano huo uliopangwa kufanyika leo.
Kikao cha kwanza kilifanyika Septemba 23 jijini Dodoma kikiwakutanisha Msajili na Jeshi la Polisi ambapo, Mkuu wa jeshi hilo IGP Simon Sirro akiwa na timu yake walihudhuria. Msajili alieleza kwamba mantiki ya kikao hicho ilikuwa ni maandalizi ya hoja za kikao cha wadau wa siasa.
Ratiba hiyo iliyotolewa na Jaji Mutungi ilionyesha Septemba 30, kilifanyika kikao kingine kati ya ofisi yake na kamati ya uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa kikiwa na lengo la kutoa nafasi kwa vyama vya siasa pia kurasimisha hoja ambazo zingejadiliwa kwenye kikao cha mwisho.
Oktoba 13, kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kilifanyika jijini Dodoma na leo yaani Oktoba 21 ndiyo ilikuwa siku ya mkutano wa wadau ambao ulipangwa kufanyika Dodoma ukiwahusisha vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wengine.
Katika kuhakikisha mkutano huo unakuwa huru, Jaji Mutungi alieleza kuwa wangetafuta mwenyekiti wa kuongoza kikao hicho, ambaye atakubaliwa na pande zote na hadi kikao hicho kinaahirishwa, taarifa zilikuwa zinaeleza kwamba Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ndiyo alitarajiwa kuongoza mkutano huo.
Mvutano wa awali ulivyokuwa
Hata hivyo, dalili za kukwama kwa mkutano huo zilianza kuonekana mapema baada ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuitaka Ofisi ya Msajili kusogeza mbele kikao hicho kwa kuwa tarehe hiyo watakuwa na mkutano wao ambao walimwalika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.
Awali Mwenyekiti wa TCD, Zitto Kabwe alisema wamepanga kufanya mkutano wao Oktoba 21 na 22 wakati ule wa Msajili ukipangwa Oktoba 20 hivyo, hawataweza kushiriki na kumtaka Msajili kusogeza mbele.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Jaffar Haniu alipoulizwa kuhusu ushiriki wa Rais kwenye mkutano huo alisema: “Mpaka sasa hatufahamu lolote, kama atashiriki, tutatoa taarifa.”
Kwa upande wake Jaji Mutungi alipoulizwa kuhusu hilo alisema hataki malumbano na kwamba, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuitisha kikao hicho.
“TCD wametangaza siku ya kufanya mkutano huo baada ya kusikia mimi nimeshapanga hivyo, kama waliona kuna hali hiyo walitakiwa waandike barua au kuja ofisini kuhusu utaratibu ulipangwa na kuona tunafanyaje,” alisema Jaji Mutungi na kuongeza: “Wasipohudhuria sawa kwa sababu sio mara ya kwanza kusema hivyo. Vyama viko 19 hata vikikataa vyama vitatu kwa sababu zao nyingine.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Bara, Benson Kigaila alipoulizwa alisisitiza kuwa chama chake hakitoshiriki kwenye mkutano huo ulioitishwa na Msajili.
“Msimamo wetu wa mwanzo bado haujabadilika, tulishasema kuwa hatutoshiriki mkutano huo lakini mambo mengine siwezi kuzungumza zaidi tunabakia hivyo,” alisema.
Chadema wamsubiri Rais Samia
Akizungumza baada ya kupata taarifa za kuahirishwa kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema sasa ni wakati wa Rais, Samia Suluhu Hassan kupanga ratiba ya kukutana na vyama vya siasa katika kipindi hiki.
Alisema wanatarajia pia kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) atamfutia mashitaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili awe huru kutekeleza majukumu yake na kushiriki kwenye mkutano huo.
CUF wasikitika
Katibu Mkuu wa CUF, Haroub Mohamed alisema ni jambo la kusikitisha mkutano huo kuahirishwa na inaonyesha kwamba hawako makini katika maandalizi yao.
Alisema chama chake kiliamua kushiriki mkutano huo baada ya kukaa kikao chao Oktoba 11 na kutoa mapendekezo ambayo waliyawasilisha kwa Msajili naye akakubali kuyafanyia kazi.
NCCR- Mageuzi
Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho, Edward Simbeye alimtaka Jaji Mutungi kuzingatia ushauri uliotolewa juzi na chama hicho wa kuufanya uwe shirikishi kwa vyama vingi zaidi.
“Huwezi kuitisha mkutano wakati watu hawaelewani, miongoni mwa vyama bado kuna sintofahamu, sasa lazima iwepo namna bora ya kutibu makovu kisha ndiyo kikao kiitishwe, hili jambo la msingi. Wajipe muda waangalie namna ya kufanya,” alisema Simbeye.
ACT – Wazalendo watoa kauli
Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu alisema; “Tumepata taarifa leo (jana) asubuhi kuhusu kuahirishwa kwa kikao. Lakini, sisi ni wanasiasa tutaendelea kufanya shughuli zetu wakati tunasubiria kikao kingine, tuna imani polisi hawatatusumbua.”
Kauli ya mchambuzi wa siasa
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk Paul Loisulie alisema ile picha ya wadau wakubwa kuamua kuususia mkutano huo, huenda ni moja ya sababu za kuahirishwa kwake kwa kuwa utakosa uhalali hata kama watashiriki wadau wengine.
Dk Loisulie alisema katika mkutano huo, wadau wenye nafasi ya kipekee ni vyama vya siasa hasa Chadema, NCCR Mageuzi, ACT - Wazalendo na CUF na kukosekana kwao kungepunguza mantiki ya mkutano huo aliosema ni muhimu kwa afya ya nchi.