WAGANGA wa tiba asili katika kijiji cha Kata ya Gambosi,wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wamemuomba Askofu Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu awaombee ili mwaka huu waweze kupata mvua ya kutosha kwa ajili ya kilimo.
Ombi hilo wameliwasilisha wakati alipokutana na Askofu huo jana kijijini hapo walipozungumza mambo mbalimbali ikiwamo kudumisha mila na desturi za kisukuma pamoja na kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19, kupiga vita ramli chonganishi.
Katika mkutano huo ulifanyika viwanja vya kanisa Katoliki Kigango cha Gamboshi, pamoja na ombi hilo, waganga hao wamemuomba Askofu huyo kuwasaidia kuwajengea ofisi katika kijiji hicho ili kutambulika rasmi na kufanya kazi zao katika eneo moja.
“Mwashamu Baba Askofu tunashukuru sana kukutana na sisi na kufika kijijini kwetu, hii ni neema kubwa sana, tunakuomba tunapoelekea msimu mpya wa kilimo utuombee kwenye kijiji chetu tuweze kupata mvua ya kutosha mwaka huu,” amesema Isabile Magaja.
“ Watu wamekuwa wakitambua Gamboshi kama kijiji cha uchawi Tanzania, lakini jambo hilo siyo kweli, hapa ni amani na upendo, tunashukuru Askofu kwa kuja hapa kisha kukutana na sisi,” amesema Mwenyekiti wa waganga hao, Saguda Busaliguka.
Kwa upande wake Askofu Sangu, akizungumza katika mkutano huo, amewataka waganga hao kuwa kielelezo kikubwa kwa jamii katika kutunza na kuenzi mila na desturi za kisikuma.
“Kupitia kazi yenu mnayo nafasi kubwa kwenye jamii kuhimiza kulinda mila na desturi, kupiga vita mambo maovu kama mauaji ya albino, mauaji ya wazee na vikongwe, lakini pia kupiga vita utoaji wa mimba wanawake.
“ Mungu ametuumba binadamu wote sawa, kuwaua albino, kutoa mimba ni kumkosea Mungu, nyie mnafanya kazi hizi kwa wema, mnatibu watu kwa miti shamba jambo jema hata kwa Mungu, lakini ni wajibu wetu kupiga vita matukio haya,” amesema Askofu Sangu.
Katika hatua nyingine, kingozi huyo wa dini amewataka wananchi wa kijiji hicho pamoja na waganga wa tiba asili, kujenga utamaduni wa kupeleka watoto shule na siyo kuwafanyisha kazi za nyumbani.