Watu 187 waliotekwa nyara Nigeria waokolewa





Polisi katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Nigeria la Zamfara wanasema vikosi vya usalama vimewaokoa karibu waathiriwa 200 wa utekaji nyara kutoka msitu katika eneo la jimbo la Maradun.
Haya yanajiri wakati vikosi vya usalama vya Nigeria vikiimarisha operesheni dhidi ya magenge yenye silaha yanayohusika na visa vingi vya utekaji nyara katika eneo hilo.

Katika taarifa msemaji wa polisi anasema wahasiriwa waliookolewa wakiwemo wanawake na watoto waliotekwa nyara wiki kadhaa zilizopita kutoka vijiji kadhaa vya jimbo hilo. Waathiriwa 187 waliookolewa na wamekabidhiwa kwa serikali ya jimbo kwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kuungana tena na familia zao.

Katika picha zilizotolewa na mamlaka, mateka walioachiliwa walikuwa wakionekana wamechoka huku nguo walizovalia zikiwa zimechanika .

Hali iliyosababisha uokoaji wao katika Msitu wa Tsibiri bado haijafahamika lakini polisi wanasema wahasiriwa waliokolewa ‘bila masharti yoyote. ''

Mamlaka imefunga huduma za mtandao na simu za rununu jimboni tangu Julai kama sehemu ya juhudi za kupambana na magenge yenye silaha yanayofanya mauaji na utekaji nyara - yakilenga watoto wa shule, jamii na wasafiri.

Licha ya operesheni za kijeshi zinazoendelea ambazo viongozi wanasema zinatoa mafanikio, kumekuwa na ripoti za kuendelea kushambuliwa kwa vijiji na watu wenye silaha na karibu wanakijiji 30 waliuawa mapema wiki hii katika majimbo ya Zamfara na Sokoto.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad