Waziri Gwajima Kumuwakilisha Rais Samia Kongamano La Tatu La Kimataifa La Wanawake Nchini Urusi

 


Na WAMJW -St. Petersburg-Urusi

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la tatu la Kimataifa la Wanawake litakalofanyika nchini Urusi kwa siku tatu kuanzia Oktoba 13-15, 2021.


Akiwa nchini Urusi, Dkt. Gwajima atashiriki katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Wanawake tarehe 13 Oktoba 2021 ambapo ataonesha namna Tanzania ilivyofanikiwa katika kuwa na usawa wa Kijinsia, kuwainua Wanawake Kiuchumi na kutambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa.


Dkt. Gwajima anashiriki katika Kongamano hilo ikiwa ni mwelekeo na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha uwepo wa usawa wa Kijinsia na uwezeshaji wa Wanawake katika nyanja mbalimbali.


Aidha, lengo kuu la Kongamano hili ni kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya Dunia kuonesha mchango wa wanawake katika maendeleo na kuhakikisha kunakuwa na usawa wa Kijinsia.



Vile vile, Dkt. Gwajima atakutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Afya wa Urusi kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika Sekta ya Afya yakiwemo mapambano dhidi ya Virusi vya UVIKO19 duniani.

Kongamano hili litaambatana na Mikutano mbalimbali inayolenga masuala kadhaa yakiwemo mapambano dhidi ya Virusi vya UVIKO19, Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi na kuwezesha usawa wa Kijinsia.

Kongamano la Kimataifa la Wanawake nchini Urusi litajumuisha Viongozi kutoka Mataifa mbalimbali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Wabunge, Mashirika ya Kimataifa, Wakuu wa Mitandao ya Kimataifa ya Wanawake na Wawakilishi wa makampuni ya kibiashara duniani.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad