Shirika la Afya Ulimwenguni – (WHO) limetoa wito kwa nchi tajiri kuachana na usambazaji wa chanjo za Virusi vya Corona kwa faida ya nchi maskini.
Akizungumza jana usiku katika Mkutano wa Kilele wa Afya Duniani Mjini Berlin, Ujerumani, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema janga la corona litamalizika pale ulimwengu utakapoamua kulimaliza.
Amesema huku kukiwa na karibu vifo 50,000 kwa wiki, janga hilo bado lipo mbali kuisha.
Ghebreyesus amesema nchi ambazo tayari zimefikisha kiwango cha utoaji chanjo cha asilimia 40 – zikiwemo nchi zote za kundi la G20 – zinapaswa kuacha mpango wa Umoja wa Mataifa wa utoaji chanjo wa COVAX au mpango wa Umoja wa Afrika AVAT kuchukua usukani katika usambazaji wa chanjo.
Ameonya kuwa hakuna nchi inayoweza kumaliza kivyake janga la corona ulimwenguni.
Mkutano wa Afya Duniani Mjini Berlin ulianza jana na utaendelea hadi kesho Jumanne na pia katika mfumo wa kidijitali.