Mtu mmoja amefariki papo hapo na mwingine kujeruhiwa baada ya pikipiki waliyokua wakisafiria kugongwa na basi la kampuni ya Sauli.
Ajali hiyo imetokea usiku huu eneo la Kwa Mathias wilayani Kibaha, Pwani wakati basi lenye namba za usajili T668 DTF mali ya kampuni ya SAULI likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam kugonga bodaboda.
Mmoja wa mashuhuda Athuman Ramadhani amedai kuwa basi hilo ambalo lilikuwa limeongozana na magari mengine na ilipofika eneo pacha la barabara jirani na kituo cha daladala Kwa Mathias lilianza kuyapita magari mengine ambapo moja wapo iliyokua mbele ilihamia njia ya pembeni inayotumiwa na magari yanayoshusha abiria.
Wakati gari hilo iliposimama kushusha abiria, ndipo bodaboda yenye namba MC 606 CAQ ikiwa na abiria mwanamke ikakatisha mbele yake huku SAULI iliyokua imeshaanza kuyapita magari mengine ikiwa mwendo kasi na ndipo ilipokutana na pikipiki na kuigongwa ambapo, iliiburuza na kuingia uvunguni mwa basi hilo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Pwani, Edson Mwakihaba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja abiria wa bodaboda aliyefariki kuwa ni Emma Mgole (37) mkazi wa Kwa Mathias huku dereva wa bodaboda hiyo Edwin Rodrick akijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Tumbi kwa matibabu ya haraka.
Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa Rodrick amehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzira, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Dereva wa basi la Sauli, Tito Gadau (32) anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo, baadhi ya vijana waliokua jirani na eneo hilo wamelishambulia basi hilo kwa mawe na kusababisha uharibifu mkubwa.