Askari Wageuza Wizi wa Simu Mradi Binafsi



Moshi. Baadhi ya askari polisi katika idara ya upelelezi nchini wanadaiwa kuanzisha utaratibu wa kuwatoza fedha watu wanaoibiwa simu na vifaa vingine vya kielektroniki kama kompyuta na tablet, wakiwaeleza kuwa fedha hizo ni gharama za ufuatiliaji.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wengi wa walioibiwa vifaa hivyo, hasa mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam na kuripoti polisi wakitaka vifuatiliwe kujua vilipo au vinatumika katika namba na mazingira gani, walitakiwa kutoa kati ya Sh50,000 na Sh150, 000 kulingana na thamani yake.

Utaratibu uliozoeleka ni kuwa ndani ya vituo vya polisi na ofisi za upelelezi wa mikoa vipo vitengo vya upelelezi wa makosa ya kimtandao, ambao baadhi yao ndio wana mawasiliano na kampuni za simu.

Utaratibu huo unadaiwa kuwapo katika mikoa mingi nchini ambapo baadhi ya wapelelezi wamehalalisha malipo hayo, kama “gharama” za kufuatilia simu hizo.


Uchunguzi huo unabainisha kuwa matarajio ya watu wengi kuwa usajili wa simu ungewezesha upatikanaji wake kirahisi hayajatimia kutokana na baadhi ya askari kulichukulia kama mradi binafsi.

Baadhi ya simu zinazoibwa nchini, polisi hufanikiwa kuzipata baada ya mmiliki wake kutakiwa kuwasilisha namba ya utambuzi (IMEI), ambapo polisi hufuatilia na kubaini mtu anayeitumia, namba yake na mahali alipo, lakini ni nadra watu hao kufikishwa mahakamani kwa kuwa kesi nyingi huishia mikononi mwa mpelelezi.

Alipoulizwa kuhusu tabia hiyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura alisema malalamikio hayo waulizwe makamanda wa polisi wa mikoa.


“Piga simu kwenye hiyo mikoa kama hayo yapo na tuhuma zake zinashughulikiwaje na kama askari wanaruhusiwa kufanya hivyo, mimi si msemaji wa mkoa, piga simu kwenye mikoa hiyo,” alisema Wambura.

Walioombwa fedha wafunguka

Baadhi ya walioibiwa simu wamedai wamekuwa wakitozwa fedha kulingana na gharama za kifaa husika, mfano gharama za kufuatilia simu ya Tecno au Intel hazipo sawa na iPhones, Oppo au Samsung.

Mmoja wa wanaodai kuombwa fedha ni Gabriel Ulomi, mkazi wa Kiusa Manispaa ya Moshi, ambaye aliibiwa simu aina ya Samsung katika eneo la stendi ndogo ya mabasi yaendayo Holili, Oktoba 29 mwaka huu.

Alisema alifanya jitihada za kupata simu hiyo ikiwa ni pamoja na kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Moshi kitengo cha wizi wa mtandao ambapo alitakiwa kulipa Sh80, 000 kwa ajili ya ufuatiliaji, ambazo fedha hizo hazikuwa na risiti ya kiserikali.


“Nilipofika pale nikajieleza niakambiwa nitoe Sh80, 000 nikatoa lakini baada ya siku moja nikaambiwa niongeze Sh40, 000 kwa kuwa simu imeonekana nje ya mji, hivyo ni gharama zaidi kuifuatilia,” alidai Ulomi.

Hata hivyo, alidai baada ya kuongeza kiwango hicho c baada ya siku mbili aliambiwa simu imeonekana katika mji mdogo wa Himo ambako hata hivyo haikupatikana tena kama alivyoahidiwa na fedha hazikurejeshwa.

Ulomi aliiomba Serikali iweke suala hilo kihalali na kisheria ili isionekane kama kitengo cha watu kujinufaisha ilhali waliopata hasara wanashindwa kunufaika kwa kurejeshea vifaa vyao.

Alishauri taasisi za bima kuwasaidia wananchi wanaomiliki simu janja kwa kuanzisha utaratibu wa kuzikatia bima ili pindi zinapoibiwa au kuharibika bima ifanye kazi kama inavyofanya katika vyombo vya moto.


Kwa upande wake, Jesca Elisamahe mkazi wa mji mdogo wa Boma Ng’ombe wilayani Hai, alidai aliporwa mkoba wenye simu na fedha kiasi cha Sh300, 000 wakati akitokea katika sherehe ya harusi usiku

Jesca alidai alienda polisi na kuambiwa atoe Sh100, 000 ili kutafuta simu hiyo na kwamba alipozitoa baada ya wiki moja aliambiwa simu inasomeka eneo la Machame ,hivyo aongeze Sh20,000 kwa ajili ya mafuta.

“Baada ya wiki niliambiwa simu inasomeka Machame nikaambiwa nitoe tena hela ya mafuta ya gari nilitoa Sh20, 000. Mtuhumiwa alikamatwa na simu niliipata na mhusika alirejesha gharama zangu zote nilizotumia katika kufuatilia, ila zile Sh300, 000 zilishaenda kwenye matumizi,” alidai mwananchi huyo.

Mlalamikaji mwingine ni mkazi wa Wilaya ya Siha, Bahati Chume, aliyedai aliibiwa simu yake yenye thamani ya Sh40,000 na kwamba alipofika kituo cha polisi wilayani humo aliambiwa atoe Sh130,000 kwa ajili ya ufuatiliaji.

“Simu nimenunua bei ndogo lakini bei ya kuitafuta pale polisi ni kubwa sana, tunaomba Serikali kupitia kitengo hicho itusaidie kwa kuwa wananchi wengi wanashindwa kutoa gharama za kufuatilia,” alidai Chume.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad