Dar es Salaam. Balozi mstaafu, Patrick Tsere amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na kufanya mazungumzo na wadau wanaotaka Katiba mpya ili kupata mwafaka wa kitaifa.
Kauli ya Tsere, aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Malawi imekuja wakati kukiwa na harakati mbalimbali za madai ya Katiba, huku Rais Samia, aliyeingia madarakani Machi mwaka huu akiwataka wenye madai hayo wamwache kwanza ajenge uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Tsere alisema angekuwa mshauri wa Serikali, angeshauri kuitwa kwa wote wanaotaka Katiba mpya kwa ajili ya kubadilishana mawazo ili kupunguza joto lililopo sasa.
“Mazungumzo hayo ya kirafiki tu, yanaweza kupunguza joto lililopo sasa, yaani ni kama ambavyo Jakaya (Rais mstaafu Jakaya Kikwete) alivyokuwa akifanya.
“Alikuwa akiwaita kina Mbowe (Freeman- Mwenyekiti wa Chadema) na kukaa nao pamoja si kupoteza ajenda, bali kupunguza tu joto,” alisema Tsere.
Huku akionyesha kusikitishwa na hatua ya kudhibitiwa kwa wanaodai Katiba mpya, balozi Tsere alisema, “leo hii hata mtu akisema hebu tupitie kidogo au tuzungumze kuhusu Katiba watu hawataki!
“Mimi nafikiri Rais awaite hao watu, yaani wadau wote kwa maana vyama vyote vya siasa kwa lengo la kuzungumza nao na ieleweke siyo kikao rasmi, bali ni kuzungumza kwanza kama rafiki.”
Juni 28 mwaka huu, wakati akijibu maswali mbalimbali ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini aliokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema: “Naomba nipeni muda nisimamishe nchi kwanza kiuchumi. Tuite wawekezaji wawekeze ajira zipatikane uchumi ufunguke, halafu tutashughulikia Katiba, tutashughulikia mikutano ya hadhara wakati ukifika”.
Balozi Tsere, ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, ameifananisha vuguvugu ya sasa ya madai ya Katiba na ya madai ya Katiba mpya yaliyoibuka miaka ya 1990, kabla ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kuunda Tume ya Jaji Francis Nyalali kuwauliza Watanzania utayari wao mwaka 1992.
Balozi Tsere alisema licha ya matokeo kuonyesha kuwa Watanzania wengi bado walikuwa wakihitaji mfumo wa chama kimoja, Mwalimu Julius Nyerere alishauri kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi.
“Taarifa ya Tume ilieleza kuwa asilimia 80 ya Watanzania hawakutaka vyama vingi na asilimia 55 ya hiyo 80 ya waliotaka chama kimoja ukiitafsiri ilikuwa inataka vyama vingi.
“Mzee Nyerere alikuwa na akili sana, akaishauri Serikali isiangalie hawa ishirini tu kwamba ndio wanataka vyama vingi na hawa asilimia 55 waangalieni maana hoja zao zinafanana,” alisema Tsere.
Alisisitiza kuwa, licha ya uchache wa waliokuwa wakitaka mfumo wa vyama vingi, bado walipewa nafasi.
“Sasa tukubaliane kwamba ni asilimia 20, kwani wachache hawapaswi kusikilizwa? Wanafaa kusikilizwa, hivyo turuhusu vyama vingi, nasema hicho kitendo alichofanya kwa maana ya ushauri aliotoa Nyerere ndio umeisaidia CCM ibaki mpaka leo madarakani,” alisema Tsere.
Alisema kama Serikali ya wakati ule ingekataa kuanzisha mfumo wa vyama vingi bado vuguvugu lingeendelea kama lilivyo suala la Katiba.
“Tunajaribu kunyamazisha lakini nafikiri huko mbeleni itafika tu litafumuka. Yaani huko siku za usoni itafika tu, tena kitu kidogo tu kinaweza kikapita na kufumua jambo hili kwa ukubwa.
“Mimi sipuuzi kabisa suala hili la Katiba na ingekuwa ni mimi ndio ningetoa huo ushauri ila nafahamu kuwa mamlaka iliyopo inajua mengi kuliko mimi ambaye nipo nje ya mfumo kwa sasa, kwa hiyo nimesema haya kwa namna ninavyoona mimi,” alisema.
Kazi ya ubalozi
Kuhusu kazi yake ya ubalozi nchini Malawi, Tsere alieleza jinsi alivyoshughulikia suala la mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Alisema mwaka 2012 baada ya kugundua uwepo wa changamoto hiyo, iliundwa tume maalumu kwa lengo la kuangalia mipaka na kukubaliana kuiweka.
“Baada ya kazi kumalizika Tanzania ilituma ujumbe Malawi kuomba mkutano wa kupitia taarifa, lakini Malawi walikataa, niliamua kukutana na Waziri Peter Mutharika kabla ya kuwa Rais, aliahidi kuwa utafanyika lakini kwa bahati mbaya mwaka 2014 Mutharika alifariki dunia kabla ya kufikia muafaka.
“Baadaye aliingia Rais Joyce Banda nikaamua kwenda kuonana na Waziri Chiuma, ambaye alisema hakuna shida, watakuja Tanzania kufanya mkutano na ulifanyika lakini wakati wa kupitia ajenda ili zipitishwe na kupokea taarifa za wataalamu waziri huyo aligoma kupokea taarifa hiyo, akisema hao wataalamu hawana mamlaka na kusema suala la mpaka lilishamalizika,” alisema.
Tsere alisema wakati ule Malawi ilikomalia mpaka chini ya Ziwa Nyasa, jambo ambalo Tanzania walilipinga, kwani maji ya ziwa yalikuwa yakisogea na ziwa kutanuka.
“Niliamua kukaa na waziri wao, wakati ule alikuwa Chiume kuzungumza tukiwa wawili na akaeleza kuwa kisiasa wakikubaliana na Tanzania imekula kwao kwa sababu Wamalawi wote wanajua hili Ziwa la Nyasa ni lao na wao ndio walivyofundishwa hivyo.
“Hawawezi kukubaliana na Tanzania katika hoja zao, bora waende Mahakama ya Kitaifa ambayo kama itaamua na kusema Tanzania ina hoja wao hawatakuwa na shida, bali watakwenda kuwaambia wananchi wao walipambana lakini imeshindikana kwa sababu Mahakama imeamua, hivyo wakubali tu,” alisema.
Hata hivyo, alisema haelewi nini kilitokea baada ya wao kuondoka, lakini anafahamu kuwa awamu ya tano ilivyoingia madarakani labda iliona haina haja ya kulizungumzia suala hilo.
“Baada ya awamu ya tano kuanza, jambo hilo halikuwahi kuzungumzwa, nafikiri waliona labda halina maana ilimradi watu wetu wanatembeleana, ndege zinapita hakuna vita, lakini ukweli ni kwamba upande wa Malawi wanaamini kuwa chini ya Ziwa Nyasa upande ambao tunasema ni wa kwetu Tanzania kuna mafuta, ndio yapo,” alisema Tsere.