Rais Joe Biden wa Marekani amesema familia za watoto waliotenganishwa na wazazi wao katika mpaka wa Marekani na Mexico, wakati wa utawala wa Trump zinapaswa kulipwa fidia.
Biden anayasema hayo katika kipindi ambacho wizara yake yenye dhamana ya kusimamia haki ikiwa katika mchakato wa mazungumzo na familia zilizoathirika.
Akipaza sauti yake katika jambo hilo, amesema pasipo kujali mazingira, wale wote waliochukuliwa watoto kwa zingatio la sera ya Trump ya kuzitenganisha familia, ikiwa na shabaha ya kuzuia familia kuingia kinyume cha sheria watapaswa kulipwa.
Ndani ya kipindi kifupi baada ya kuingia madarakani, Biden aliunda kikosi kazi kwa lengo la kuwaunganisha mamia ya watoto na wazazi wao ambao waliathiriwa na sera ambayo ilitumika kwa miezi kadhaa, mwaka 2018, ambayo ilizusha kilio cha ndani na kimataifa.