Binti Mvutaji wa Shisha Asimulia Alivyoharibikiwa




NI hali ya kusikitisha ingawa inabaki palepale kwamba ndio hali halisi.

Kisa na mkasa cha mwanamama kijana anayejitambulisha kuwa ni mtumiaji dawa za kulevya, akiweka msimamo kuwa hawezi kuacha wala hana mpango huo.

Akiwa mwenyeji wa Nipashe kwenye mazungumzo maalum, Rehema (siyo jina lake halisi), mkazi wa Sinza Kumekucha mkoani Dar es Salaam, kwa sasa yupo katika awamu ya tatu ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya sheesha (shisha), anakiri anachokitumia sasa, ndio hasa kinampatia kile atakacho kwa asilimia zote.
Rehema ambaye ni mchangamfu na anayejiamini, anataja hatua ya kwanza kwamba alianza na bangi, tena kwa kuiga, kisha akahamia kwenye sigara kabla ya kujisogeza katika uvutaji wa shisha, anayoipa cheo haina mpinzani, akijinasibu inampa raha aitakayo na hatoiacha ng'o!

Ameingiaje kwenye urahibu huo? Rehema ambaye kwa sasa hana kazi maalum baada ya kuachishwa kwenye taasisi binafsi (anaitaja), anasimulia mwanzo wa safari yake mwaka 2019, akiwa mkazi wa Kariakoo katikati ya Mtaa wa Livingstone na Congo, alijikuta anaingia kwenye mkumbo wa kuvuta bangi kutokana na mazoea ya majirani aliokuwa akishinda nao barazani jioni baada ya kazi.

Kwa mujibu wa dada huyo mwenye umri miaka 23 sasa, wakati huo anaanza alikuwa 'kijana mbichi' wa miaka 21, akawa mwanachama rasmi wa 'Kariakoo barazani', akipata elimu ya kina ya matumizi ya bangi.


Rehema anasema wakati huo kila alipokuwa akitoka kazini baada ya kupumzika jua lilipotua, ilikuwa ni desturi kwa wakazi wa mitaa hiyo kukaa vibarazani kubadilishana mawazo na hapo ndipo alipoanza kujifunza taratibu bangi.

"Nilikuwa ninawaona vijana wenzangu waliokuwa majirani zangu Kariakoo wanapokaa barazani jioni, wanatengeneza misokoto ya bangi kisha wanaanza kuvuta, nikavutiwa nao nikawa ninawaomba ninavuta.

"Baada ya muda nikazoea nikawa teja, yaani kila nilipojisikia kutamani kuacha nilishindwa maana kuna wakati yaani si umeshapata 'ka-kiu' kunywa pombe, basi nami nikawa ninapata kiu ya kuvuta bangi. Nilijiwekea utaratibu nikiwa ninavuta mara mbili kwa wiki na uvutaji wangu ulikuwa ni kuanzia jioni kabla sijaenda kwenye starehe zangu," anasimulia.


Binti huyo anasema amedumu kuwa mvuta bangi kwa takriban miaka miwili, taratibu akajikuta ndani ya mtiririko wa awamu nyingine ya kuanza kuvuta sigara, ingawa anakiri haikuwa kila mara.

Ndani ya safari hiyo, kuanzia mwaka jana akajitosa kwenye aina tofauti, akivuta shisha, burudani yake anayoisifia inamkosha zaidi kuliko zote zilizotangulia. Anasema kwa mara ya kwanza alipoona watu wanaivuta klabu, alitamani kujaribu kujua ilivyo.

Akirejea alikotoka, Rehema anasimulia alipokuwa katika awamu za bangi na sigara, staili ya matumizi yake haikuishia katika 'kijiwe' barazani pekee, bali aliendeleza penye kumbi za starehe na hasa klabu za usiku alikopenda kwenda siku nyingi.

Huku akifafanua hadi sasa anavutia huko kilevi chake cha sasa - shisha, anakiri kuwa kama ilivyokuwa barazani, huko nako kuna wadau wengine wavutaji ambao wamezama zaidi kwenye shisha, wengi ni vijana wenzake.


"Nimejikuta nami nimezama huko. Kwa sasa nimehamia kwenye shisha, kila nikienda klabu lazima nitafute Sh. 10,000 hadi 25,000 kwa ajili ya kuvuta shisha.

"Shisha ina gharama kidogo. Zipo klabu nyingine zinaiuza mpaka Sh. 60,000 na kuendelea. Nikitoa Sh. 10,000 tunakaa watu watatu kila mmoja akiwa amelipa, tunavuta kwa kutumia mirija maalum. Tunavuta, tunajisikia raha, ni ulevi ambao ukitoka nje kwenye hewa nyingine unajisikia poa," anasimulia.

Rehema ana ufafanuzi kuhusu ulevi huo anaosisitiza umewateka vijana wengi, kwamba wanapenda shisha kwa sababu imetengenezwa kwa kuwekewa ladha tofauti zinazowavutia.

"Ipo yenye ladha ya minti, stroberi, ladha ya ndizi na kama zilivyo bia, shisha nayo imewekewa kiwango cha ulevi, zipo zenye kiwango kikubwa cha ulevi na cha kiasi," anafafanua.


MADHARA YA SHISHA

Binti huyo anakiri kuwa, hafahamu kemikali na malighafi zilizomo ndani yake na kama zina madhara kiafya.

Hata hivyo, ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2019 kuhusu athari za tumbaku na sigara za kielektroniki (ikiwamo shisha), ilibaini sigara za kielektroniki zina kiwango kikubwa cha nicotine, kemikali ambayo ni chanjo cha maradhi ya saratani ya mapafu na magonjwa ya moyo.

Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Dk. Peter Mfisi, ana angalizo katika hilo, akionya: “Dawa za kulevya zipo za aina mbili; halali na zisizo halali ambazo zinadhibitiwa. Mfano, heroine, cocaine mirungi, bangi na nyingine, tunafanya kazi ya kuzidhibiti, zimeorodheshwa kwenye jedwali. Vitu kama pombe, tumbaku, kuberi vinalevya lakini havidhibitiwi na sheria yetu namba 5 ya mwaka 2015 ya kudhibiti dawa za kulevya.”

Anasema Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilifanya utafiti kuhusu shisha na kubaini ina kiwango kikubwa cha nicotine.

"Mtu akivuta shisha mara moja ni sawa umevuta sigara 200. Wizara ya Afya ililiona hilo, ikaomba mamlaka zinazohusika ikatazwe,” anasema na kukiri hadi sasa hakuna sheria inayozuia matumizi ya shisha nchini, hivyo mamlaka yao kushindwa kudhibiti mwenendo wa biashara na matumizi yake.


Kamishna Mfisi katika himitisho lake, anaishauri kuchukua hatua kwa kupeleka muswada wa sheria bungeni kudhibiti biashara na matumizi ya shisha nchini, akibainisha kuwapo kundi kubwa la vijana wanaovuta shisha kwenye miji mikubwa nchini.

WIZARA YAKIRI TATIZO

Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Omary Ubuguyu, anasema matumizi ya shisha yana madhara makubwa kiafya.

"Tumbaku unayoichemsha ili uisisimue mwili maana yake ni kwamba mtu anayetumia shisha anamzidi anayetumia tumbaku ya kuvuta kwa maana ya athari za kemikali zinazosababisha sumu ni kichocheo cha magonjwa yasiyoambukiza kama saratani za aina zote.

"Kuharibika mishipa damu na kuongeza hatari ya kuharibu figo na moyo. Matumizi ya shisha ni mlango wa matumizi huria ya dawa za kulevya, wengine wana tabia ya kuchanganya ndani yake cocaine, heroine na bangi. Kubwa kuliko yote ni madhara yake mtu ana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya saratani, kisukari, figo na moyo,” anafafanua.

Dk. Ubuguyu anasema ipo Sheria ya Kuzuia Matumizi Holela ya Tumbaku ya Mwaka 2004, lakini wakati inatungwa shisha haikuwa sehemu ya bidhaa za tumbaku zilizokatazwa kwa mujibu wa sheria hiyo.

"Bahati nzuri, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepewa jukumu la udhibiti na matumizi ya tumbaku. Hao wana nafasi ya kusaidia.

"Kwenye hili la matumizi ya shisha ni kama umenipa taarifa, nitawakumbusha TMDA kulipitia hilo kisheria kwa sababu wamepewa mamlaka ya dawa na vifaa tiba," anasema.

Nipashe inafika mezani kwa Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza, ambaye katika ufafanuzi wake anasema tangu Aprili 30, mwaka huu walipokabidhiwa rasmi majukumu ya kudhibiti matumizi holela ya tumbaku, wameanza kwa kutoa elimu kwa umma ili kupunguza idadi ya waathirika wa bidhaa za tumbaku, ikiwamo shisha.

VIFO KWA MAMILIONI

Mei 31, mwaka huu, Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani, alibainisha kuwa takribani watu milioni sita hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake kama sigara na shisha na wakati mwingine kuvuta moshi unaotoka kwa mvutaji huku baadhi yao wakiwa ni watoto ambao hupoteza maisha kwa asilimia 28, wanawake asilimia sita na wanaume asilimia moja.

Waziri alirejea ubashiri wa kisayansi kwamba vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku vitaongezeka na kufika zaidi ya milioni nane kwa mwaka ifikapo 2030, ambao ni mwaka wa ukomo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Vilevile, takwimu za WHO za mwaka 2003 zinaonyesha kila baada ya sekunde 10, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na matatizo yanayosababishwa na matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Kwa lugha rahisi ya mazungumzo, hiyo ni sawa na vifo vya watu sita katika kila dakika, sawa na vifo 60 kwa saa na vifo 1,440 kwa siku.

Novemba 3, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janab, akizungumza katika mkutano wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania (TTCF), alisema kati ya wagonjwa 100 wa moyo, 25 wanapata maradhi hayo kutokana na matumizi ya tumbaku.

Profesa Jabab pia alibainisha kuwa asilimia 80 ya wanaougua saratani, chanzo chake ni matumizi ya tumbaku.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad