BREAKING NEWS: Milipuko miwili imetokea katika Mji mkuu wa Kampala nchini Uganda, mapema leo Jumanne, Novemba 16, 2021 huku watu wawili wakidaiwa kupoteza Maisha kutokana na milipuko hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinaeleza kuwa mlipuko wa kwanza umetokea kwenye jengo la maduka karibu na Kituo Kikuu cha Polisi na mwingine karibu na Jengo la Bunge.
Majengo yaliyopo karibu na maeneo hayo yametikisika wakati milipuko hiyo ilipoanza. Video zimesambaa miotandaoni zikionyesha magari yakiwaka moto nje ya jengo la Bima baada ya milipuko hiyo.
Imeelezwa pia kwamba, Spika na Maofisa wa Bunge wameokolewa na jeshi la polisi waliokuwa wamezingira eneo hilo.
Mwezi uliopita, milipuko miwili tofauti nchini humo iliua watu wawili. Mmoja ulimuua mhudumu katika baa na mwingine, mshambuliaji wa kujitoa mhanga ambaye alikuwa ameingiza vilipuzi kwenye basi.
Mamlaka nchini humo zimeshutumu milipuko hiyo ya Oktoba dhidi ya kundi la waasi wa Kiislamu lenye makao yake makuu nchini Uganda, DR Congo, Allied Democratic Forces. Takriban watu 50 wamekamatwa, na wengine kushtakiwa mahakamani, tangu matukio hayo ya hivi majuzi.