Bunge Lasitisha Shughuli zake, Hali Bado Tete Kampala, Mabomu Usipime




Naibu spika wa Bunge, Anita Among amesitisha shughuli za Bunge na kuwataka wabunge kubaki majumbani wakati hali ya usalama ikiwa tete katika jiji la Kampala kufuatia milipuko miwili.


Uamuzi huo umetolewa dakika chache baada ya kutokea milipuko hiyo katika maeneo mawili tofauti leo Jumanne asubuhi.



Mlipuko wa kwanza ulitokea katikati ya jiji na dakika chache baadaye mwingine ulilipuka katika barabara ya Bunge na kugonga jengo la bima la Jubilee ambalo pia lina ofisi za mkaguzi mkuu wa ofisi za Serikali.



Mlipuko mwingine uliripotiwa karibu na Mnara wa Kooki, mkabala na Kituo Kikuu cha Polisi. Watu wengi wanadaiwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika milipuko hiyo.



Shughuli zote za Bunge za siku ya leo zimesitishwa, kuanzia kwenye vikao vya kamati. Wabunge na watumishi wengine wa Bunge wametakiwa kubaki nyumbani.



“Nimeagizwa na Naibu spika wa Bunge nikutaarifu kuwa leo hakutakuwa na kikao cha Bunge, unashauriwa usiende kwenye viwanja vya Bunge kwani vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa ya kurejesha utulivu ndani ya Bunge.



“Mpaka mtakaposhauriwa vinginevyo, naomba mkae nyumbani na wale walio katika viwanja vya Bunge watulie na wasubiri ushauri wa namna ya kuondoka,” inasomeka taarifa iliyotolewa na karani wa Bunge, Adolf Mwesige.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad