Mkazi wa kitongoji cha Ujerumani, Baraka Kulwa aliyetaka kumuoa mwanafunzi wa darasa la sita mwenye miaka 14 pamoja na mama mzazi wa binti huyo, wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wilaya kwa tuhuma za kumuoa na kumuozesha mwanafunzi huyo.
Wakisomewa maelezo ya awali mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa Serikali, Damas Chonya mbele ya hakimu mkazi, Jullius Mhanusi, imedaiwa walitenda kosa hilo Novembea 10, 2021.
Amesema walikamatwa na polisi wakiwa kwenye harusi ya kimila baada ya polisi kupewa taarifa za siri na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuwa kuna mwanafunzi anaozeshwa na ndipo walianza ufuatiliaji na kufanikisha kuwakamata wakiwa kwenye sherehe.
Chonya aliwataja waliokamatwa kuwa ni bwana harusi, Baraka Kulwa (26), Rashid Saidi (40), mama wa binti huyo, Stumai Sakenge (35), mpambe wa bwana harusi, Sadam Shaban (18) pamoja na mama wa bwana harusi, Sandu Sandu Maduhu(55) wote wakazi wa kitongoji cha Ujerumani.
Baada ya kusomewa mashtaka wote walikana kosa lao na mwendesha mashtaka amesema upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwamba kesi hiyo itaendelea Novemba 25, 2021 na washtakiwa walirudishwa rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.