Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kutetea haki za wazee ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa mafao ya wastaafu.
Chama hicho pia kitaweka utaratibu mzuri wa kisheria wa huduma za afya na kupata uwakilishi katika vyombo vya uwakilishi, ikiwamo Bunge na mabaraza ya madiwani.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, wilayani Kasulu leo, alipokuwa akizungumza na Baraza la Wazee wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Ziara hiyo pia ilihusisha pia mikoa ya Kagera, Geita, Kigoma, Katavi na Tabora ili kukagua uhai, uimara wa chama na utekelezaji wa Ilani ya Chama ya Mwaka 2020/2025.
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM Taifa Shaka Handu Shaka, Chongolo amesema kundi la wazee linastahili kutungiwa sheria kama ile ya mtoto iliyotungwa kwa namba Namba 21 ya Mwaka 2009, inayolinda haki za mtoto na kuelezea wajibu wa mzazi.
Alisema kundi la wazee linastahili kuwa na sheria mahsusi itakayolinda haki zao na kuweka wajibu wa kuwalazimisha watoto kuwatunza wazee wao ili kuwabana vijana wanaowatelekeza wazazi wao baada ya kunufaika na wajibu wa wazazi wao katika makuzi yao.
“Nakubaliana na ninyi kuwa Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 ni nzuri sana lakini imechukua muda mrefu kuwa sheria, Kwa namna hali inavyokwenda ni bora tukafikiria kuwa na sheria itakayolinda haki za wazee na kuelezea wajibu wa watoto kwa wazazi wao
“Tayari tuna sheria inayokutaka wewe mzazi kuwajibika kwa mtoto kuhakikisha anapata haki zake lakini wapo watoto wanaowatelekeza wazazi wao wakiwa wamezeeka.”alisema Chongolo.
Amesema kwa namna ile ile ilivyotungwa sheria inayowawajibisha wazazi basi iwepo na ile itakayowawajibisha watoto kuwatunza wazee wao badala ya kuwasahau.
Akizungumzia kuhusu wazee kuwakilishwa Bungeni, Chongolo alisema kuwa kundi hilo linastahili kuwekewa utaratibu huo, akisistiza kuwa iwapo mchakato wa Serikali utachukua muda mrefu basi CCM inaweza kuweka suala hilo kupitia taratibu za ndani ya chama kama ambavyo makundi mengine kama wanawake, wenye ulemavu, vijana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, yalivyo na uwakilishi bungeni.
Chongolo amesema kupitia utaratibu wa kisheria unaoandaliwa na Serikali wa kuwasilisha muswada wa Bima ya Afya kwa wote, itakuwa ni fursa nzuri kuhakikisha kundi la wazee linapata huduma za afya kwa uhakika kwa sababu watapata matibabu ya magonjwa yanayowasumbua uzeeni baada ya kulitumikia taifa.