Chanzo Cha Upungufu wa Maji Mto Ruvu na Uhaba wa Maji Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani



Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani hivi karibuni walikumbwa na kadhia ya kukosa Maji katika maeneo yao, huku Mamlaka husika zinazosimamia upatikanaji wake zikitoa taarifa juu ya upungufu wa rasilimali Maji katika Mto Ruvu ambao ni chanzo kikubwa cha Maji katika maeneo hayo.

Kutokana na upungufu huo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ambao wanahusika katika usambazaji walisikika wakitangaza mgao katika maeneo mbalimbali hususani katika mikoa hiyo ya Dar es Salaam, Pwani sambamba na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutoa taarifa ya mgao wa umeme kutokana kupungua kwa Maji kwa kiasi kikubwa katika vyanzo vyake.

Hali hiyo ya upungufu wa mtiririko wa Maji katika maeneo hayo hususani Mto Ruvu, imetajwa kuwa ni Mabadiliko ya Tabia nchi, shughuli mbalimbali za Binadamu karibu na vyanzo vya Maji, pia kusababisha chanzo kikubwa cha upungufu huo katika mito, mabwawa mbalimbali yanayotegemewa kutoa huduma za Maji kwa matumizi mbalimbali.

Novemba 16 - 20, 2021 Bodi ya Maji, Bonde la Wami/Ruvu lilifanya oparesheni maalum katika Mto Ruvu, baada ya agizo la Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Novemba 15, 2021 alipotembelea Mitambo ya kuzalisha Maji, Ruvu Juu na Chini, ambapo aliagiza Bodi hiyo kuangalia vizuri vyanzo vya Maji hususani Mto Ruvu ambapo ni chanzo kikubwa cha Maji katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Bonde la Wami/Ruvu walisikia agizo hilo na Afisa Maji Msaidizi, mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Halima Faraji, Jumanne ya Novemba 16, 2021, Afisa huyo Msaidizi wa Maji na timu yake sambamba na timu ya Waandishi wa Habari waliongozana katika maeneo ya mkoa wa Pwani, kwa ajili ya kuanza kutekeleza agizo hilo la Waziri Mkuu wa Tanzania.

Kikosi kazi cha Maafisa na Wataalamu wa Maji wa Bonde la Wami/Ruvu mkoa wa Dar es Salaam kikiongozwa na Bi. Halima Faraji kilifanya jitihada kubwa kupita katika Vitongoji, Kata na Vijiji mbalimbali katika mkoa wa Pwani kutoa elimu ya umuhimu wa kulinda vyanzo vya Maji, kudhibiti upotevu wa Maji hayo katika vyanzo vyake kwa kuwashirikisha Wenyeviti, Watendaji na Wananchi wa maeneo hayo.


MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mabadiliko ya Tabia nchi ni moja ya sababu iliyotajwa kupunguza au kukausha Maji, Mto Ruvu. Hali ya janga la Ukame na kukosekana Mvua kwa muda mrefu imeelezwa kusababisha hali hiyo ya ukosefu wa Maji. Kutokana na sababu hiyo, Jamii imekumbushwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa kufanya ibada na Dua ili kuleta neema ya Mvua katika maeneo hayo yenye Ukame.

Hali hiyo ya ukame imesababisha maji kupungua mtoni na hivyo kuathiri uzalishaji wa maji katika Mitambo ya Maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu inayomilikiwa na Mamlaka ya DAWASA.


UWEPO WA IDADI KUBWA YA MIFUGO MKOANI PWANI

Moja ya changamoto kubwa ambayo timu ya Bonde la Wami/Ruvu ilikutana nayo katika maeneo ya mkoa wa Pwani ni uwepo wa idadi kubwa ya Mifugo. Shughuli za ufugaji mkoa wa Pwani kwa kiasi kikubwa zinafanywa na watu wa Jamii ya kabila la Wamasai, ambao wanafuga idadi kubwa ya Ng’ombe hali inayopelekea kusababisha uharibufu wa vyanzo vya Maji kando kando ya Mto Ruvu.

Jamii ya Wamasai wengi wanafanya shughuli za ufugaji mkoani Pwani, idadi kubwa ya Mifugo yao hususani Ng’ombe wengi husababisha mmomonyoko wa kingo za Mto huo, sambamba na kupoteza kiasi kikubwa cha Maji kwa Ng’ombe hao kunywa Maji mengi zaidi ya Lita 40 hadi 60 katika Mto huo, ambao unaotegemewa na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani katika kuzalisha Maji.

Katika kutekeleza jitihada mbalimbali za kunusuru Mto Ruvu, Jamii hiyo ya Wamasai imeshauriwa kuchimba na kutumia Mabwawa binafsi (Malambo) kwa ajili ya kunyweshea Maji Mifugo yao ili kunusuru kina cha Maji katika Mto huo. Licha ya malalamiko kutoka kwa Jamii hiyo ya Wamasai kutokana na Mifugo hiyo kufa kutokana na kukosa Maji, bado imesisitizwa kuchimba Mabwawa binafsi ili kunusuru Mto Ruvu.


SHUGHULI ZA BINADAMU KANDO KANDO YA MTO RUVU

Ni sababu nyingine iliyotajwa kupunguza kiasi kikubwa cha Maji katika Mto Ruvu. Shughuli mbalimbali za binadamu, hususani shughuli za Kilimo na Umwagiliaji kando kando ya Mto huo bila kuzingatia Mita 60 Kisheria kutoka Mtoni, kumetajwa kusababisha kadhia hiyo ya ukosefu wa Maji.

Shughuli za binadamu si Kilimo na Umwagiliaji pekee, bali hata shughuli za Ufuaji Nguo, Kuosha Vyombo na Kuogelea ndani ya Mto huo kumesababisha kupungua kwa kiasi cha Maji.

Mfano, Maafisa hao wa Bonde la Wami/Ruvu walimkamata raia mmoja wa China (51) ambaye alikuwa anafanya shughuli za Kilimo na Umwagiliaji akiwa na mashine kubwa ya kuvuta Maji kwenye mto Ruvu akipeleka Maji hayo katika Shamba lake la zaidi ya Hekari 50 katika eneo la Kata ya Kidogozero mkoani humo.


MKUU WA MKOA WA PWANI, KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WATEMBELEA VYANZO VYA MAJI

Pia katika kuhakikisha agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan linatekelezwa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abuubakari Kunenge na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo ilitembelea vyanzo mbalimbali vya Maji na kutoa elimu, kudhibiti shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wananchi kando kando ya Mto Ruvu na vyanzo vingine vya Maji.

RC Kunenge alitoa maagizo mbalimbali ikiwemo kudhibiti Mifugo wanaoharibu Mto Ruvu na kupunguza kiwango cha Maji katika Mto huo. Pia Kunenge aliagiza kuchukuliwa hatua Wafugaji wanaingiza Mifugo yao kiholela katika Mashamba ndani ya mkoa huo.

Bodi ya Maji, Bonde la Wami/Ruvu kwa mamlaka iliyopewa kusimamia Rasilimali za Maji chini ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009. Kifungu cha 43(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11, 2009 kinamtaka mtu yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua, na kutumia maji kutoka kwenye chanzo cha maji juu au chini ya ardhi au kujenga muundombinu wowote kwa lengo la kutumia maji ni lazima aombe kibali cha kutumia maji hayo.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad