Wasanii wawili wakubwa nchini Tanzania Diamond Platnumz na Harmonize wapo kikaangoni baada ya kupeana skendo nzito ya matumizi ya madawa ya kulevya
Hivi karibuni, Diamond alirusha kijembe kwa msanii ambaye hakumtaja akimtaka kuacha mihadarati (bangi) ambayo ni miongoni mwa makundi ya dawa za kulevya
Katika kujibu kijembe hicho, Harmonize naye akaanika jambo zito kwamba msanii huyo ameona shilingi milioni 600 alizolipa ili kuondoka WCB zimeishia kwenye matumizi ya unga na ndiyo maana amedhoofika mwili
Gazeti la IJUMAA limewatafuta maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ili kujua kama wamesikia tuhuma hizo nzito na kama kuwa hatua yoyote wamechukua
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye ofisi hiyo nyeti, tayari wasanii hao wanafuatiliwa kwa ukaribu na kikosi kazi cha mamlaka hiyo iliyo chini ya Kamishna Jenerali Gerald Musabila Kusaya
Habari za kiintelijensia zinadai kwamba, Diamond na Harmonize ni wasanii wenye wafuasi wengi na wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa hivyo ni lazima kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo ili kupata ukweli kisha hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa kitengo hicho ambaye hakupenda kuchorwa jina gazetini, alisema jambo hilo lipo kwenye uchunguzi hivyo asingeweza kutoa habari zozote kwa kuwa siyo msemaji wa mamlaka hiyo
Ofisa huyo anasema si mara ya kwanza kutolewa tuhuma kama hizo kwa wasanii, lakini mara zote wamekuwa wakifuatilia na kubaini ukweli
Si mara ya kwanza kwa Diamond kuhusishwa na dawa za kulevya ambapo awali alidaiwa kuhusika na biashara hiyo haramu, lakini sasa anatuhumiwa kutumia
Mmoja wa mameneja wa Diamond Mkubwa Fella aliwahi kuliambia Gazeti la IJUMAA kwamba tuhuma hizo hazikuwa na ukweli wowote ndiyo maana baada ya uchunguzi msanii huyo hakufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu mashitaka hayo
Kwa upande wake Harmonize, mara kadhaa amekuwa akidaiwa kujihusisha na uvutaji wa bangi kiasi cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuagiza akaripoti Polisi kwa maelezo zaidi.