MWAMBA ni Myao wa Tunduru. Kabla ya kuanza kuimba Singeli alianza kuigiza kwa miaka sita, lakini hakupata nafasi ya kutoka na kuwa mkubwa kama alivyo sasa hivyo akaacha kuigiza.
Huku na huku akakutana na Mkubwa Fella. Akajiunga na Kundi la Mkubwa na Wanawe. Akaanza kuimba Bongo Fleva. Baadaye akaona ni ngumu kutoka kirahisi kwenye Bongo Fleva. Akatumbukia kunako Singeli.
Ngoma yake ya kwanza ni Yanga japokuwa haikujulikana kama ni yake kutokana na Msaga Sumu kuiimba mara kwa mara na yeye kujulikana.
Jamaa hakuwa na la kufanya kwa sababu hakuwa na pesa hivyo aliamua kupotezea japokuwa alikuwa akiutumia kwa sababu alikuwa amesikia wimbo wake ukiimbwa na mtu mwingine kwenye matamasha makubwa.
Baada ya hapo aliendelea kutoa ngoma nyingine kama Makabila, Hujaulamba na nyingine nyingi.
Huyu si mwingine bali ni mkali wa Singeli anayetamba na ngoma yake mpya ya Nikizipata.
Jina halisi ni Abdallah Ahmed lakini lile la kutafutia rizki ni Dulla Makabila.
Jamaa anasema moja kati ya vitu ambavyo Watanzania wanapaswa kujivunia ni pamoja na muziki wa Singeli kwa sababu sasa hivi ameweza kuupeleka duniani mwenyewe akianzia Uturuki.
Katika mahojiano maalum (exclusive) na Gazeti la IJUMAA, Dullah anafunguka mambo mengi ikiwemo ishu ya kukesha kwa waganga kuwaloga watu mbalimbali;
IJUMAA: Mambo vipi Dulla?
DULLA MAKABILA: Salama kabisa uzima upo.
IJUMAA: Hongera tunaona umefikisha muziki wako hadi Uturuki…
DULLA MAKABILA: Namshukuru sana Mungu kwa kila hatua ninayopiga kwenye muziki wangu maana bila yeye siwezi kufanya chochote. Kingine ni mashabiki wangu nawapenda sana na pia nashukuru kwa sapoti yao kwangu na wasanii wenzangu, Wolper na wengine ambao wameweza kunisapoti kwa hili.
IJUMAA: Unajisikia kuweza kufikisha muziki wa Singeli kimataifa?
DULLA MAKABILA: Nilikuwa natamani sana siku moja ndoto yangu ije itimie na sasa huu ndiyo muda rasmi wa muziki wa Singeli kwenda kimataifa.
IJUMAA: Naona wasanii wenzako wa Singeli watapata la kuzungumza maana siyo jambo la mchezo, singeli ilikuwa inafanywa kama muziki wa Uswahilini…
DULLA MAKABILA: Mimi ndiye Mfalme wa Singeli, naichukua Singeli, naipeleka duniani na nimeanzia Uturuki.
IJUMAA: Hongera sana kwa hatua hiyo ya udhubutu kwani siyo jambo dogo.
DULLA MAKABILA: Ahsante sana.
IJUMAA: Ila nasikia Dulla unaloga sana, je ni kweli?
DULLA MAKABILA: (anacheka) nani amekuambia? Basi huyo aliyekuambia kwamba mimi naloga atakuwa alijaribu kuniloga akanishindwa.
IJUMAA: Hivi umeacha siku hizi kwenda kwa waganga wa kienyeji?
DULLA MAKABILA: Naenda tena sana tu!
IJUMAA: Bado hujapunguza tu kwenda huko?
DULLA MAKABILA: Nisiwe muongo kwa kweli, siwezi kupunguza au kuacha.
IJUMAA: Kwa nini sasa usipunguze?
DULLA MAKABILA: Nina sababu gani za kupunguza?
IJUMAA: Vipi kuhusu ishu yako na Baba Levo na Wasafi imekaaje?
DULLA MAKABILA: Baba Levo mimi sina shida naye kabisa. Kwanza mimi ni shabiki wake sana hata yeye huwa analitambua hilo. Kuna kipindi nilimkosea, niliumia sana, unajua kuna mtu hakupi pesa ya kodi wala ya kula, lakini unamkubali sasa, ndiyo ilivyo kwa mimi na yeye.
IJUMAA: Mmekuwa mkishirikiana kwenye mambo mengi sana, vipi kuna mpango wa kuachia kazi yoyote na yeye?
DULLA MAKABILA: Mipango ipo sana tu ila kikubwa ni kumuomba Mungu kila kitu kiweze kwenda kama kilivyopangwa.
IJUMAA: inasemeka kwamba Dulla umetengwa na Diamond na Wasafi ndiyo maana unahaha kwa mahasimu wake, huna makao, mara EFM, mara Konde Gang, vipi kwani hebu tujuze kilichopo nyuma ya pazia…
DULLA MAKABILA: Unajua nini tusimuangalie Majizzo wala Mondi, wale wakikutana ni marafiki, hata mimi kujimaliza kwenye wimbo wangu najuta maana kuna siku hadi niliwahi kumwambia Mondi yaani mimi najipinda kuimba kwenye nyimbo kumbe ninyi ni wana, mnapiga hadi picha ya pamoja…
IJUMAA: Alikujibuje yeye Mondi kuhusiana na kupiga picha na Majizzo?
DULLA MAKABILA: Sikumbuki.
IJUMAA: Vipi sasa kuhusiana na wewe na Mondi?
DULLA MAKABILA: Hatuna tatizo.
IJUMAA: Kivipi na habari zinasambaa kwamba sasa hivi hakuna mawasiliano mazuri?
DULLA MAKABILA: Tupo sawa kabisa, hatuna neon. Kama kuna ambacho niliropoka siyo vya kweli, mimi huwa nikiona waandishi wa habari naropokwa sana.
IJUMAA: Ahsante sana pia tunaomba urudi salama Tanzania.
DULLA MAKABILA: Ahsante pia.
MAKALA: KHADIJA BAKARI