Fahamu wakati sahihi kufunga tumbo la uzazi


Dar es Salaam. Ni jambo lililozoeleka kwa wanawake kufunga tumbo baada ya kujifungua wakilenga kulirudisha katika hali yake ya kawaida.

Inaelezwa kuwa wengine hufunga kwa kanga, mitandio mikubwa au kuvaa mkanda.

Na ikumbukwe kuwa utamaduni huu ulianza tangu enzi za mabibi na dhana hii ilijengeka kwa wanawake wote kuwa ukifunga tumbo baada tu ya kujifungua, litanywea.

Lakini wataalamu wa afya wanasema dhana hiyo si sahihi, bali wanasema kisayansi, tumbo huwa linanywea lenyewe baada ya mama kujifungua.

Wanasema hakuna ulazima wa kulifunga, bali dawa rahisi ya kukiondoa kitambi cha ujauzito ni lishe na mazoezi katika siku za mwanzo baada ya kujifungua.

Hata hivyo, wanasema mama anaweza kulifunga tumbo baada ya siku 42 kupita tangu ajifungue (japo si lazima), ili kuruhusu kizazi kirudi chenyewe bila athari yoyote.

Wakati wataalamu wakitoa maoni hayo, baadhi ya wanawake ambao wamepitia hatua hiyo waliozungumza na Mwananchi wanasema licha ya kufunga matumbo, wapo baadhi yao hukumbana na changamoto za aina tofauti.

“Nina watoto watatu na kila nilipokuwa ninajifungua nilifunga tumbo. Sikusubiri siku 40 zipite lakini nimekuwa nikipata shida kidogo, mara nyingi huwa ninashindwa kupumua vizuri,” anasema Rose Konga.

Hata hivyo, utafiti wa kisayansi unaonyesha kuna faida chache, lakini pia kuna hasara nyingi zaidi za ufungaji wa tumbo baada ya kujifungua

Wanasayansi wazungumza

Baadhi ya wanasayansi wametaja sababu hasa inayomfanya mama kutanuka tumbo kuwa ni mabadiliko baada ya homoni zinazoachiwa kuruhusu misuli ya tumbo kutanuka ili kuruhusu mtoto kukua.

Akizungumzia hali hiyo, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Aga Khan, Jane Muzo anasema kitu kingine kinachotokea ni pingili za mgongo kuruhusu tumbo kuwa kubwa na kumbeba mtoto kwa uzito wake.

Hivyo anasema kwenye ufungaji wa tumbo la mama aliyetoka kujifungua, hasara zinakuwa nyingi kuliko faida ambayo ni kurudisha misuli katika hali yake ya kawaida, ingawa baada ya muda, mama hujikuta ameharibu misuli ya ndani.

Pia anasema hasara nyingine inayotajwa na wanasayansi ni kupunguza mfumo wa upumuaji.

Dk Muzo anasema kwa sababu kuna msuli unaitwa ‘diaphragm’ ambao uko juu ya tumbo, huo una asilimia 60 ambayo inamfanya mwanadamu aweze kupumua, hivyo unapokuwa umefungwa unaweza kumzuia mama kupumua vizuri.

Naye Mkunga mtaalamu, Agnes Ndunguru anasema kufunga tumbo kwa mama aliyetoka kujifungua ni makosa.

Anasema kufanya hivyo kunaingilia kazi inayotakiwa kufanywa na mwili, hivyo kumuumiza mama.

“Tunakutana na madhara mengi kwa kinamama waliotoka kujifungua wakafunga kanga au matumbo kwa lengo la kuyarudisha. Wengi ile kanga hufunga kwenye kizazi, ile haitakiwi. Mama anatakiwa kila baada ya dakika 15 tunashauri awe ana massage eneo la kizazi kwa kutumia mikono yake mwenyewe,” anasema Agnes.

Anasema kufunga tumbo mara baada ya kutoka kujifungua ni kukilazimisha kile kizazi kurudi kwenye pango, wakati kizazi kinakuwa kinarudi taratibu hakihitaji kulazimishwa.

Anasema hiyo nayo inasababisha kutokwa damu nyingi kwa sababu inakwenda kusukuma sehemu ya kizazi ambayo kwa muda ule inahitaji kutulia na kujiminya yenyewe iweze kurudi katika pango la nyonga.

“Kitu cha muhimu hapo kinamama wazingatie mazoezi ambayo ni mara baada ya kujifungua.”

Hata hivyo, Agnes anasema mama aliyetoka kujifungua anaruhusiwa kufunga tumbo lake siku 42 baada ya kujifungua siyo mbaya, kwa kuwa wakati huo kizazi huwa kimeshashuka na kimerudi kwenye pango la nyonga.

“Sasa huyu mama anayefunga wakati huu anakuwa hapambani tena na mji wa mimba, bali lile eneo la juu ambapo wengine huwa wanafunga huku wanafanya mazoezi, ile inaruhusiwa na ni nzuri zaidi kutumia hii mikanda ya kisasa kwa sababu kanga material yake siyo kitu rafiki.

“Wengine wametumia kanga wakapata michubuko kwa ajili ya kufunga muda mrefu kwa sababu inazuia mzunguko wa damu kupita kwenye lile eneo, kwa hiyo inatengeneza kidonda,” anasema.

Agnes anashauri mama aliyetoka kujifungua asubiri mpaka siku 42 zipite ndipo aweze sasa kufunga tumbo kwa ajili tu ya kukaza misuli ya eneo la tumbo, pamoja na mazoezi lakini inatakiwa atumie mikanda maalumu.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, Isaya Mhando anasema muda wa kufunga tumbo ukifika inategemea na tumbo la mama husika na uzito wa mtoto aliyemzaa.

“Mara nyingi huwa inatokana na ukubwa wa mtoto aliyembeba, mwanamke aliyebeba mtoto mwenye uzito wa kilogramu 4 mpaka 5 tumbo hutanuka zaidi ikilinganishwa na yule aliyebeba mtoto wa uzito wa kawaida, yaani kuanzia kilogramu 2.5 hadi 3 na zaidi,” alisema.

Anasema mama akishajifungua unapomwambia akaze tumbo inasaidia kufanya tumbo lirudi katika nafasi yake na misuli kukaza.

“Baada ya kujifungua misuli inayozunguka tumbo inakua imelegea, unapomwambia mama afunge kanga au mtandio mkubwa ile inamsaidia kutoa ushirikiano ‘ku support’ misuli kurudi katika hali yake ya awali na hii tunafanya kwa kinamama wote.

“Wale wanaozaa watoto wakubwa wanakuwa wametanuka zaidi hivyo ni muhimu kufanya zoezi hili,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mhando alisema hiyo ni tofauti kwa wanawake ambao ni wanene na wenye matumbo makubwa ambao huzaa watoto wenye uzito mdogo. “Tunawashauri wale wenye uzito mkubwa mama apunguze uzito wake awe na uzito wa kawaida kabla hajabeba mimba.”

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Aga Khan, Jane Muzo anasema kiafya inashauriwa mama kufunga tumbo, huku akisema wale waliotoka kujifungua inasaidia kupunguza maumivu na mfumo wa damu uweze kuzunguka vizuri.

Anasema misuli na sehemu zilizofanyiwa upasuaji hupona haraka na hupunguza uvimbe uliopo nje ya ngozi kwa mama katika mshono.

“Mama akishajifungua hapa katikati kuna misuli miwili inapita katikati inakwenda chini huwa ina tabia ya kutanuka na kulegea, hivyo inasaidia kuirudisha katika hali yake na pia kumsaidia mama asitokwe na mkojo bila kujijua, yaani inasaidia kukaza misuli ya chini maeneo ya kibofu,” anasema.

Dk Muzo anashauri mama akijifungua wakati wa kufunga mkanda ukifika asiwe mtu wa kukaa tu au kulala wakati wote, bali anapaswa kujishughulisha ili kuzuia tumbo lisitepete.

“Anapojishughulisha misuli inakaza vizuri na inarudi katika hali ya kawaida. Zamani walikuwa wanafunga kwa ajili ya kuzuia damu isitoke nyingi, lakini walikuwa wanakaza misuli, lakini watafiti wameona ule mkanda wanaofunga na wasiofunga hakuna tofauti, wapo kinamama ambao hawajafunga na wako vizuri,” alisema Dk Muzo.

Mazoezi yanayoshauriwa

Hata hivyo wataalamu hao wameshauri ni vema mama akatumia mazoezi ya kukaza misuli siku 42 baada ya kujifungua ili kurudisha mwili katika umbile lake la awali.

Mama aliyejifungua anaweza kufunga mkanda baada ya kushauriana na mtaalamu aina ya mkanda na sehemu ya kufunga.

Wataalamu wanasema kuna mikanda mingine unaweza kufunga chini ya kitovu na kuna mwingine unafunga chini ya maziwa kwa lengo la kutaka kuondoa kiribatumbo cha chini ya kitovu, pia kuna mikanda mingine ni ya kuimarisha pingili za mgongo na tumbo.

Pia wameshauri kina mama wanaojifungua badala ya kufunga mikanda wafanye mazoezi ya tumbo kwa kuelekezwa na mtaalamu wa afya.

“Yapo maeneo mengi yanatoa huduma za mazoezi kulingana na uchunguzi atakaofanyiwa mama hivyo, kila mama anafanya mazoezi kulingana na kazi anayofanya, kubadilisha aina ya ulaji.

Kinamama wa ofisini hufundishwa namna ya kufanya mazoezi ya tumbo ‘isometric exercise’ ambayo hufanywa wakati wa kusimama, kukaa au kutembea kwa kuvuta tumbo ndani kisha kuachia kwa kuhesabu 1-15 mazoezi ambayo mama anaweza kufanya mwenyewe eneo lolote alilopo.

Aidha walitaja mazoezi mengine ‘sit ups’ ambayo hutolewa baada ya kufanya uchunguzi sahihi kwa mhusika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad