Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema watuhumiwa wanatakiwa kuheshimiwa na kutendewa haki kama watu wasio na hatia mpaka itakapobainika vinginevyo.
IGP Sirro alitoa kauli hiyo jana, wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN-Women) pamoja na Mtandao wa polisi wanawake ndani ya jeshi hilo yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Moshi (TPS).
Mafunzo hayo yalienda sambamba na uzinduzi wa kitabu chenye mwongozo wa namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake.
“Hakuna kitu muhimu kwetu kama kusimamia sheria na kutenda haki, kuwa wanyenyekevu na kuheshimu watu. Sisi leo tumevaa majoho haya na kesho tunarudisha kwa wenyewe na wenyewe ni Watanzania ambao wanalipa kodi ambayo inatufanya tufanye kazi.
Pamoja na mambo mengine, alisema zipo jitihada za utatuzi wa changamoto mbalimbali ndani ya jeshi hilo, ikiwamo masuala ya utumishi .
“Nitajitahidi katika upangaji wa nafasi za utendaji kazi kwa maofisa wanaondelea na mafunzo vyuoni wanaomaliza hivi karibuni ili madawati haya ya jinsia yaweze kupata uwakilishi kuanzia ngazi za vituo, wilaya hadi mkoa,” alisema.
Alisema kwa sasa zipo changamoto za masuala ya ugaidi, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake ambavyo vinapaswa kushughulikiwa kikamilifu.
“Natambua mtandao wa polisi wanawake ni moja ya maboresho yaliyofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania ili kushughulikia masuala ya askari wa kike pamoja na kuzuia masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, mtandao wa polisi wanawake sasa umerasimishwa kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ukatili,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya mwakilishi mkaazi msaidizi wa UN Women, Lucy Tesha alisema wamekuwa wakifanya kazi ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake katika ngazi ya kimataifa na kitaifa.
“Tunalishukuru Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo wanashirikiana na sisi, ambapo tangu madawati kuanzishwa mwaka 2008 mmekuwa mfano bora wa uendeshaji wa dawati la jinsia kwa weledi katika kukabiliana na matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii” alisema Lucy.