MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuongezeka kwa vipindi vya joto nchini Tanzania ambavyo vitaendelea hadi Desemba 2021 huku mtawanyiko wa mvua ukitarajiwa kuongezeka vilevile mionzi ya jua la utosi ikiondoka.
Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri, Samwel Mbuya amesema uwepo wa jua la utosi tropiki ya kaprikoni huja na vipindi vya joto kali na hujirudia tena mwezi February wakati jua la utosi likielekea tropiki ya kansa.
“Viwango vya joto vimeongezeka kwa kiwango kikubwa sana na baadhi ya maeneo Nchini yameripoti kiwango cha nyuzi joto zaidi ya kile cha kawaida katika mwezi Novemba. Mfano, mbali na kuwa na mlima mrefu barani Afrika na misitu mikubwa Kilimanjaro ndio mkoa unaoongoza kwa joto kal.
“Kilimanjaro joto limefikia nyuzi joto 36.4 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.6 kutoka kiwango cha kawaida cha wastani, maeneo mengine ukanda wa Pwani hali ndio kama hivyo zimeongezeka kwa takribani nyuzi joto 2.2 mpaka 4.6 juu ya kiwacho cha kawaida kwa mwezi Novemba.
“Kwa eneo hili la ukanda wa Pwani pia kuna changamoto ya kwamba tupo karibu na bahari kwahiyo viwango vya unyevunyevu kutoka kwenye bahari vinakua vipo juu na hivyo kusababisha kuwepo kwa hali ya fukuto ambayo inaongeza hali ambayo tunaipata sasa hivi ya joto katika maeneo ya mikoa hii ya ukanda wa Pwani.
Aidha, kiwango cha juu cha joto katika mkoa wa Dar es salaam kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika mkoa wa Ruvuma kimefikia nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3,” amesema Samwel Mbuya kutoka TMA.