K-Mziwanda Kutoka Kuwa Konda Hadi Uhamasishaji Simba






CHAMPIONI Jumatano, limekusogezea simulizi mzuri ya shabiki wa Simba, mwanadada ambaye kwa sasa amekuwa
maarufu mitandaoni kutokana na maneno yake.

 

Ni yule aliyekuwa mhamasishaji Simba Day, lakini ni yule aliyezungumza akiwa na Mwijaku kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Mwijaku akitoa ahadi ya kutembea bila nguo kitaani.Dada huyo anajulikana kama K Mziwanda, mwandishi na mtangazaji ambaye kwa sasa yupo Mbengo TV.



Championi limepiga naye stori nakujua mengi kuhusu maisha yake.“Jina langu halisi ni Kessy au Kuruthum Hassan. Nimezaliwa mtoto wa kike pekee kwenye familia ya watoto wanne ya Mzee Hassan Omary Rhumba.“Tulizaliwa kwenye Kijiji cha Maramba jijini Tanga.
 

Mimi ni Mdigo wa Duga Maforoni mjukuu wa Mzee Beja wengi wananiita hivyo huko nyumbani.“Nina kaka zangu wanne, mimi ndiye wa mwisho kuzaliwa.

 

ALIVYOINGIA KWENYE MICHEZO
“Kuhusu michezo nilianza kupenda toka nikiwa mdogo nikiwa nasoma shule ya msingi.“Wakati ule Halima
Mchuka (marehemu) akiwa mtangazaji pekee wa mpira mwanamke redioni, kina Sued Mwinyi wakitangaza
mpira kwa uhodari mkubwa Mbali na hayo pia Simba ndiyo ilifanya niongeze mahaba kweye soka, wakati ule Simba
ya moto, kina Ulimboka Mwakingwe, Athuman Idd ‘Chuji’, wakaja kina Patrick Mafisango na wengine.

 

ALIWAHI KUCHEZA SOKA
“Huu mpira mbali ya kuushabikia, nimeucheza sana, wakati nipo Shule ya Sekondari Agreement, pale
nilikuwa kiranja mkuu na ikawa rahisi kuucheza toka kidato cha kwanza hadi cha tatu.

“Nilibahatika kuwa mchezaji muhimu na kiongozi kwenye timu ya shule ya wanawake, juhudi
zangu zikaonekana hadi kuchaguliwa kuwa kwenye timu ya Mkoa wa Tanga kwenye mashindano ya Umiseta.

 

MAMA YAKE AMUWEKEA NGUMU
“Mama alikuwa hapendi nicheze mpira kabisa na ikalazimika niache hayo mambo ya kucheza baada ya kufika kidato
cha nne. Mtu pekee aliyekuwa ananisapoti alikuwa ni baba.

NI MTU WA DINI
“Nimelelewa kwenye mazingira ya dini sana, kwetu ilikuwa ni bora usiende shule ila uende madrasa.

ALIKUWA NGUMI MKONONI
“Makuzi yangu yalikuwa yamejawa ugomvi na ukorofi, ingawa napenda sana utani na ucheshi.

 

MARAFIKI ZAKE MASELA TU
“Sina marafiki wengi wanawake, napenda kukaa sana na wanaume, kwa sababu wanawake mara nyingi ni
ngumu kujadili vitu vya msingi.

 

KWAO NI SIMBA TU
“Ukimtoa baba, wengine wote pale nyumbani ni mashabiki wa Simba hadi mama, baba alijitahidi sana
kunivuta niwe shabiki wa Yanga lakini ikashindikana.

 

KUMBE ILIBIDI AWE MJEDA
“Baada ya kumaliza shule, baba alinifanyia mpango ili niende jeshini, kila kitu kilikuwa tayari ulikuwa
unasubiriwa muda tu ufike.


“Baadae ikabidi nije Dar, lengo ilikuwa ni kuja kusomea udereva ili niende jeshini nikiwa na fani nyingine mbali na soka tu.

 

AIBUKIA KWENYE UTANGAZAJI WA RADIO
“Wakati nasomea udereva, Times FM walikuwa wameanzisha shindano la kusaka mtangazaji wa redio. Nikaona
huenda ikawa fursa kwangu.


“Kwa sababu nilikuwa napenda sana kusikiliza redio na kuna wakati nikiwa peke yangu nikawa najifanya
mtangazaji au kama kuna watu wamekaa sehemu nilipenda sana kuwahoji.

“Nikaenda kuchukua fomu ili niweze kushiriki na kujaribu bahati yangu. Nikakutana na watu zaidi ya 1000 ambao wanashiriki.

“Nifika hadi mchujo wa watu 30, kwa bahati mbaya nikatolewa kwenye mchujo wa kwanza wa fainali. Mashindano yalikuwa yanafanyika Dar Live Mbagala.

 

AGEUKIA UKONDA WA DALADALA
“Baada ya kushindwa kwenye mashindano ikabidi nitafute kazi ya kufanya baada ya kukaa nyumbani kwa wiki tatu,
ikabidi niwe konda wa daladala.


“Nikawa napakia abiria kutoka Buguruni kwenda Chanika (Dar), wakati mwingine tunapiga ‘root’ ya
Buguruni hadi Makumbusho, ilikuwa inanibidi niamke mapema na kuifuata gari Tabata Shule kila siku.

 

AHAMIA KWENYE SINGELI
“Nikaona ukonda wa daladala pekee hautoshi, nikahamia na kwenye Muziki wa Singeli na nikawa
nimetoa wimbo wangu kwa kwanza unaitwa Chawa.

 

SIMU YA E-FM YAMPA MCHONGO TIMES
“Ngoma yangu ya Chawa ikawa kama tundu langu la kufanya kazi Times FM, nilipokea simu ya interview (mahojiano) juu ya wimbo wangu pale E-FM.


“Wakati najiandaa kwenda kwenye interview, nikawa nimeweka ujumbe kwenye group (kundi) ambalo tulikuwemo washiriki wote wa shindano la kusaka vipaji.


“Mule kwenye group kulikuwa na viongozi pia wakubwa wa Times, kumbe wao walikuwa na mpango
wa kunichukua kwani walivutiwa sana na mimi licha ya kuwa sikufika mbali kwenye mashindano.

“Walivyoona ile taarifa ya kuwa nakwenda E-FM nafikiri walihisi naenda kufanya kazi, ikabidi wanipigie simu kuwa niende Times na wakawa wamenipa ajira moja kwa moja.


“Nilifanya kazi kwa miaka minne, nikatangaza vipindi tofautitofauti, nilianza na Goma la Uswazi, ilikuwa
mara moja kwa wiki ambayo ni Jumamosi tu.

“Wakaniongezea na Jumapili kisha baadae ikawa Ijumaa hadi Jumatatu, walipoondoka kina Dida kwenda Wasafi, ikabidi nifanye pia na Mitikisiko ya Pwani ambacho ni kipindi cha Taarabu.

“Nikapewa kipindi cha Umbea CCTV Camera, baadae nikawa nafanya na kipindi cha burudani ambacho alikuwa anafanya Idris wa Kitaa, Bongo.Com. Baadae nikaenda digital nikapewa kipindi cha Uswazi Macho kwa Macho.

 

MCHONGO WA CHUO VIPI?
“Nimesoma uandishi wa habari ngazi ya cheti, ila diploma niliishia njiani.

 

KUHUSU MUZIKI WA SINGELI
“Msanii Young Yuda ndiye aliyenifanya nipende singeli, Msaga Sumu na kaka yangu mkubwa pia.

 

KUHUSU MANARA
“Manara (Haji, msemaji wa Yanga) ni mwalimu kwangu, nimejifunza vingi kutoka kwake, nilikuwa najifunza namna
ambavyo alikuwa anapambana na watu wanaoichafua Simba.

 

ULIJISIKIAJE KUWA MC SIMBA DAY?
“Ilikuwa ni siku ya kumbukumbu kwangu, kwa sababu sikutegemea mapokezi ya mashabiki ikiwemo kuwasha taa na
kusimama kwa kauli yangu juu ya kumpokea Emmanuel Okwi.


“Nilipata pongezi nyingi sana, kutoka kwa watu mashuhuri, waandishi wakubwa na viongozi wa serikalini. Ndiyo nilipata fedha lakini haikuwa kitu juu ya heshima kubwa niliyopata ya kuwahutubia watu zaidi ya 60 pale kwa Mkapa.

 

YEYE SIYO MHAMASISHAJI
“Niliweke sawa hili, mimi siyo mhamasishaji, ila bado ni shabiki wa kawaida kama walivyo wengine. Ile
siku ilibidi kuzungumza ili kuamsha morali kwa sababu palikuwa kama pamepoa,” anamaliza K Mziwanda.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad