Mamlaka nchini Ecuador imesema kuwa kiasi cha wafungwa 68 wameuawa na wengine 25 kujeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya magenge ya uhalifu katika gereza la Guayas N1 la mji wa bandari wa Guayaquil katika Pwani ya Pacifiki.
Ofisi ya mwendesha mashtaka imesema kuwa idadi hiyo ya vifo ni kulingana na taarifa za awali na kuongeza kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu makabiliano hayo ya ghasia yalioanza siku ya Ijumaa usiku na kuendelea hadi jana asubuhi.
Hapo jana, idara ya kitaifa ya polisi imesema kuwa operesheni inaendelea katika gereza hilo la Guayas N1 kudumisha utulivu na uthabiti.
Vyombo vya habari katika eneo hilo vimenukuu polisi ikisema kuwa bunduki, bastola mbili na baruti 10 zilinaswa wakati wa operesheni yake.Aidha, jana jioni, serikali ya jimbo la Guayas, lililopo eneo la Guayaquil ilisema kuwa imerikodi mapigano mapya katika gereza hilo.