Dar es Salaam. Katika mkakati wa kupunguza riba ya mikopo inayotolewa na benki za biashara nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewatangazia kiama wafanyakazi na wakopaji wanaopindisha sheria na utaratibu kukopa.
BoT imesema imefanya uchunguzi na kubaini kati ya mambo yanayochangia riba kuwa juu ni vitendo vya baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hizo kutoa mikopo kwa kupindisha utaratibu uliopo na wakopaji kufanya udanganyifu unaozilazimu benki hizo kuweka tahadhari kwa kutoza riba kubwa.
Kwa kuutambua ukweli huo, BoT ambayo ndio mamlaka inayodhibiti sekta ya benki na taasisi zote za fedha nchini imetangaza hatua za kuwashughulikia watu wote wanaopindisha utaratibu hivyo kusababisha riba kuwa juu kwa wakopaji wengine.
Katika kutekeleza hilo, imesema itashughulika na wafanyakazi pamoja na wateja wanaoshiriki kuukiuka utaratibu uliowekwa na Serikali.
“BoT itandelea kuzikagua benki na taasisi za fedha. Iwapo itathibitika kuna mfanyakazi anahusika kutoa mikopo kwa kukiuka taratibu, kukosa uadilifu, na kushirikiana na wakopaji kutoa mikopo kiuhalifu, na vitendo vya rushwa, benki au taasisi husika itatakiwa kumchukulia hatua za kisheria mfanyakazi huyo na BoT itamfungia kuajiriwa na benki au taasisi nyingine yoyote,” amesema Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga.
Licha ya wafanyakazi hao kushiriki kupindisha sheria na utaratibu, Profesa Luoga amesema wapo wenye mikopo chechefu katika benki au taasisi nyingine hivyo kuzitaka benki wanakofanya kazi kuwasilisha taarifa zao katika taasisi za kuchakata taarifa za mikopo (credit reference bureau).
Iwapo itathibitika kuwa kushindwa kwao kurejesha mikopo waliyonayo kumetokana na uzembe, uhalifu au kukosa uadilifu, BoT imesema itawazuia wafanyakazi husika kuajiriwa katika benki au taasisi nyingine ya fedha.
Kwa wakopaji, BoT inazitaka benki na taasisi kutotoa mikopo kwa watu wasio waaminifu au ambao wanakopa kwa njia za udanganyifu na kuacha kulipa. Taarifa za wakopaji wa aina hii imesema zitatunzwa katika rejesta maalum na benki na taasisi za fedha zitapewa orodha yao kuhakikisha hawakopeshwi tena na benki wala taasisi ya fedha.
Licha ya wakopaji kutoka sekta binafsi, BoT pia imeweka utaratibu wa kushughulika na watumishi wa Serikali kwa kuzitaka benki na taasisi za fedha kuwasilisha orodha ya wenye mikopo chechefu ili hatua stahiki zichukuliwe.
Taarifa za watumishi hao, kama ilivyo kwa wakopaji na wafanyakazi wa benki wanaokiuka utaratibu, imesema zitaingizwa katika rejesta maalum na kusambazwa benki zote na kwenye taasisi za fedha kuhakikisha hawapati tena mikopo hadi watakapolipa madeni yao.
“Wananchi waliokopa watimize wajibu wao kwa kurejesha mikopo wanayokopa. Aidha, watoe taarifa benki, kwenye taasisi ya fedha au Benki Kuu kuhusu vitendo vya uhalifu au rushwa wanavyokutana navyo wanapohitaji huduma kutoka benki au taasisi ya fedha,” amesisitiza gavana kwenye taarifa aliyoitoa.
Michael Zebedayo, ofisa mwandamizi wa benki moja nchini alisema mikopo chechefu ni gonjwa linaloisumbua sekta ya fedha duniani kote ndio maana Benki ya Dunia na Shirika la fedha Duniani (IMF) wanafuatilia kwa ukaribu suala hili.
“Taifa lenye uwiano mdogo wa mikopo chechefu huonekana kuwa sekta imara ya fedha kutokana na usimamizi makini wa kuulinda uchumi wa nchi na fedha za wateja wanaoweka amana zao benki,” alisema Zebedayo.
Mara nyingi, alisema BoT huzisimamia benki na taasisi za fedha kwa kutumia sheria na kanuni zilizopo pamoja na miongozo inayotolewa na huzikagua walau mara moja kila mwaka.
“Hii ya sasa naweza kusema ni tiba ya uhakika kwa mikopo isiyolipika ambayo mara nyingi huchangiwa na wafanyakazi wa benki husika waliokosa uadilifu wakishirikiana na wakopaji wenye uwezo lakini wasiotaka kulipa mikopo yao pamoja na wakopaji wasio na sifa kukopeshwa kinyume na utaratibu hivyo kutolipa. Kwa hatua hizi, benki zitaweza kukusanya mikopo inayoshikiliwa kwa muda mrefu na wakopaji wasiotaka kulipa,” alisema Zebedayo.
Ofisa huyo, aliongeza kwamba kuondolewa kwa wafanyakazi wasio waaminifu kwenye mfumo na sekta ya benki kutaifanya iwe imara zaidi na fedha zitakazookolewa zitatumika kuziongezea uwezo wa kuwakopesha wakopaji waaminifu walio tayari kurejesha mikopo yao hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
Akizungumzia udanganyifu unaofanywa na wakopaji, Januari Mtitu, mfanyabiashara wa Kariakoo alisema hiyo ni michezo inayochezwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya wafanyabiashara na wafanyakazi wa benki husika.
“Hiyo ipo sana. Sio lazima uwe na duka au nyumba kama utaratibu unavyotaka. Watu wengi wamekopeshwa kiujanjaujanja,” alisema Mtitu.
Akitoa mfano wa tawi moja lililopo Kariakoo, alisema kulikuwa na mfanyabiashara ambaye alikuwa anashirikiana na ofisa kufanikisha mikopo hata kwa wasioona ofisi.
“Mtu anakuja dukani kwako, anasimama hapo, wanampiga picha mambo yanakuwa yameisha. Hati ya nyumba inakuwa bandia ila kila kitu kinaenda sawa. Yule jamaa (mfanyakazi wa benki) amefukuzwa kazi. Inasemekana alisababisha hasara kubwa,” alisema Mtitu.
Amina Hussein, mkulima wa mpunga wilayani Ifakara anasema ni ngumu kupata mkopo wa kilimo benki kwani masharti hayatekelezeki.
“Licha ya kuthibitisha shamba ulilonalo bado wanataka uwe umevuna na kupitishia fedha kwenye akaunti ya benki. Hawajui kuwa mchele unauzwa bila mikataba, yaani mtu amekuja anataka magunia matano unaanzaje kumwambia akuingizie hela benki wakati anayo taslimu?...huo utaratibu mimi naona ni namna tu ya kukwambia haukopesheki,” alisema Amina.
Melekezo ya BoT yametolewa siku moja baada mjadala kuibuka bungeni kuhusu riba kubwa ya mikopo inayotozwa na benki za biashara nchini, hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei.
Dk Kimei alitoa hoja hiyo miezi michache tangu BoT itoe mwongozo wa kuziongezea benki ukwasi hapo Julai. Kati ya yaliyoahidiwa ni benki hiyo kutenga Sh1 trilioni ajili ya benki zitakazokopesha esekta ya kilimo.
Hata hivyo, Dk Kimei alisema “faida imeongezeka benki kwa ajili ya wanahisa ila hakuna unafuu kwa wakopaji. Sehemu iliyobaki imeelekezwa kwenye hatifungani za Serikali.”