Mmiliki wa kampuni ya mitandao ya kijamii ya Facebook, Mark Zuckerberg huenda akalazimika kusubiri kwa muda kabla ya kuanza kutumia rasmi jina jipya la kampuni yake na nembo.
Itakumbukwa, siku chache zilizopita, Mark alitangaza kwamba wameamua kubadili jina na kuita kampuni hiyo “Meta”. Sasa imebainika kwamba kuna watu ambao wana hatimiliki ya jina hilo “Meta” na nembo yake, hivyo wanataka kulipwa dola milioni 20 ambazo ni takribani Bilioni 46 za Kitanzania kabla ya kumuachia Mark jina hilo.
Kwa mujibu wa TMZ, mnamo mwezi Agosti mwaka huu, waanzilishi wa kampuni iitwayo Meta PC walisajili nembo na jina hilo na wakapata hakimiliki. Hata hivyo ombi la wamiliki hao kwa Mark Zuckerberg la $20 Milioni bado halijajibiwa.
Maoni ya wadau wengi wanaona kwamba kiasi cha fedha ambacho wamiliki wa Meta wanadai ni kikubwa, lakini wamekitetea wakisema ikiwa watamuachia Mark Zuckerberg nembo yao watalazimika kufanya mabadiliko makubwa kwenye kampuni yao ambayo inahusika na mauzo ya tarakilishi, vipatakalishi na bidhaa nyingine za kiteknolojia.
Watalazimika kutafuta jina jingine na nembo nyingine na huenda hilo likawagharimu.