KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema malengo yao ni kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi baada mechi mbili zilizobaki za hatua ya makundi ya kufuzu kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
Poulsen ameyasema hayo leo Novemba 10,2021, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya DR Congo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Taifa Stars ipo nafasi ya kwanza katika kundi J na pointi saba sawa na Benin, DR Congo ya tatu na alama tano, huku Madagasca ambayo itakutana na Stars Novemba 14, 2021 ikiwa ya nne na pointi tatu, timu zote zimecheza mechi nne.
Kocha huyo amesema wamecheza michezo minne tayari na wanaongoza kundi, hivyo wanahitaji kuwa bora zaidi ya hapo na kufanikiwa kwenda hatua nyingine.
Ameeleza kuna vitu wamejifunza katika mchezo uliopita na DR Congo ugenini na ambao walitoka sare ya 1-1,anajua ubora wa wapinzani wao na wamekuja na mpango wa kuvuruga mipango yao lakini wamejipanga kimbinu.
“Tunaingia katika mchezo muhimu sana, DR Congo wamekija na mipango yao na sisi tuna mipango yetu, malengo ni kushinda mchezo na kumaliza wa kwanza katika kundi letu baada ya kucheza hizi mechi mbili za mwisho za makundi.
“Maandalizi yamekwenda vizuri, wachezaji wana morali kubwa na wanafurahia kuwa pamoja kwenye familia ya Taifa Stars,” amesema Poulsen.
Aidha amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo, pia kuwa nyuma ya timu siku zote katika mashindano inayoshiriki.
Kwa upande wake Nahodha wa Stars, John Bocco amesema wanaiheshimu DR Congo lakini wanaimani ya kufanya vizuri kutokana na maandalizi waliyofanya.