KIMENUKA..Anaswa na Nyara za Serikali, yamo Mafuta ya Simba



Katavi. Jeshi la polisi mkoa wa Katavi linamshikilia mkazi wa Ilunde wilaya ya Mlele, Seda Mbutula (47) kwa tuhuma za kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni mafuta ya Simba na ngozi yake akiwa amezificha kwenye mfuko nyumbani kwake.

Mbali na Nyara hizo za Serikali lakini mtuhumiwa huyo anadaiwa pia kukamatwa akiwa na ngozi ya Kakakuona, ngozi ya paka pori, vipande vinne vya meno ya ngiri na mkia wa nyumbu ambavyo kwa mujibu wa sheria ni nyara za Serikali.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Ally Makame alitoa taarifa hiyo leo Novemba 27, 2021 wakati akizungumza na wanahabari kutoa taaarifa ya mafanikio ya operesheni waliyoifanya na kuwakamata watuhumiwa wa mkosa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, alisema Mbutula alikamatwa Novemba 23,2021 saa 9:02 alasiri katika Pori la Akiba la Rungwa lililopo kata ya Ilunde na alikuwa ameficha nyara hizo ndani ya nyumba yake na kwamba anaendelea kuhojiwa.

Katika tukio lingine, Kamanda Makame alisema Novemba 24,2021 saa 11:15  jioni, polisi walimkamata Samweli Kazambi (36) mkazi wa Milala Manispaa ya Mpanda  akituhumiwa kuwa na kete 12 za bangi na mbegu zake gramu 1,000.

Kamanda Makame ametumia mkutano huo kuwasisitizia wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha katika muda maalum wa msamaha uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene.

“Zoezi hili la kusalimisha silaha limeanza Novemba 1,2021 na linatarajiwa kukamilika Novemba 30,2021 watakaosalimisha ndani ya muda  watapata msamaha wa kutoshtakiwa,”alisema Kamanda Makame akaongeza:-.

“Watakaokaidi watasakwa na kukamatwa na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Nitoe rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Katavi watoe ushirikiano kwa kuwafichua wahalifu wakiwamo wanaomiliki silaha kinyume cha sheria ili mkoa uwe salama,”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad