MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, imekataa kupokea barua ya utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Barua hiyo ni ile ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya, kwenda kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Kipolisi Ilala (RPC), Dar es Salaam, ili kumuomba baadhi ya nyaraka alizitumie kwenye kesi yake ndogo.
Nyaraka hizo alitaka kuzitumia kuthibitisha na au kutothibitisha, kama askari polisi, Ricardo Msemwa alikuwepo katika chumba cha mashtaka cha Kituo Kikuu cha Polisi Dar ea Salaam, tarehe 7 Agosti 2020.
Uamuzi huo wa kukataa, umetolewa leo Jumatatu, tarehe 29 Novemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo.
Akitoa uamuzi huo mdogo ya pingamizi la jamhuri dhidi ya barua hiyo, Jaji Tiganga amesema, mahakama imekataa kupokea barua hiyo kwa kuwa shahidi aliyeomba kuitoa hakujenga msingi wa mnyororo wa utunzwaji kielezo hiko hadi kumfikia (Chain of Custody).
Jaji Tiganga amesema, Ling’wenya alishindwa kuieleza mahakama hiyo namna barua hiyo ilivyotoka kwa naibu msajili wa mahakama hiyo kwenda kwake.
“Ni wazi sio nakala yake yeye, sababalu nakala yake yeye isingekuwa na mhuri wa naibu msajili, haya yangeweza kuthibitika kama angezungumza, angeweza kutumia nakala yake iliyotumika kum-save msajili.”
“Amekuwa mchumi wa maneno hajaeleza kwa nini barua inamhuri wa mahakama hivyo mahakama inabaki inajiuliza kilelezo anachotaka kukitoa kinafanana na kile kilichopelekwa kwa RPC Ilala. Mahakama haina majibu,” amesema
“Mahaka inaona kielelezo kilichopelekwa kwa RPC Ilala hatuwezi sema kama kinafanana na kilichopokelewa na RPC Ilala, shahidi ameshindwa ku-establish chain of custody.”
“Kwa kushindwa kutoa maelozo kwa nini kina mhuri na kama uligongwa na msajili ilikuwaje na kwa nini kilimrudia yeye. Ilikuwaje yeye hajataka kutoa kielelezo chake yeye na ku-tender kielezo cha mahakama. Shahidi ameshindwa kuthibitisha chain of custordy kwa sababu hiyo mahakama inakikataa kielezo hicho,” amesema Jaji Tiganga.
Jaji Tiganga amesema, shahidi huyo alishindwa kujenga msingi juu ya uelewa wake dhidi ya barua hiyo, kwa kuwa hajaieleza mahakama alikutana na nyaraka hiyo katika mazingira gani.
“Nakubaliana na jamhuri kwamba, shahidi alitakiwa aonyeshe kwamba yeye ana ufahamu wa kutosha kuhusiana kielelezo hiki na alipaswa kuweka msingi wakati anatoa ushahidi wake kabla ya kuomba kukitoa mahakamani.
Pili, uthibitisho mhusika aliwahi miliki kielezo, ni wazi kuona kielezo bila uthibitisho kuonesha mhusika amekimiliki kielelezo haitoshi kuthibitisha mhusika alikuwa na uwezo wa kutambua,” amesema Jaji Tiganga.
Jaji Tiganga amesema, shahidi huyo ameshindwa kujenga msingi unaonesha yeye ana uwezo wa kukitoa kielelezo hicho, kwani hajaithibitishia mahakama ana uelewa nacho wa kutosha.
“Ameshindwa kuonesha compitence yake na kielelezo kutokana na ukweli hajaeleza namna alivyooneshwa kielelezo, alikifanyia nini kama alikipitia, alisoma akaeleawa.”
“Hii mahakama inashindwa kuamini sababu anashindwa kujenga msingi kuonesha ana uwelewa nacho wa kutosha,” amesema Jaji Tiganga.
Upande wa mashtaka uliweka pingamizi dhidi ya barua hiyo Alhamisi iliyopita, baada ya Ling’wenya akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Dickson Matata, kuiomba mahakama iipokee nyaraka hiyo kama kielezo katika kesi ndogo.
Barua hiyo ya upande wa utetezi, ilidaiwa kwenda kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam, kuomba baadhi ya nyaraka ili kuthibitisha kama Askari Msemwa, alikuwa msimamizi katika chumba cha mashtaka (CRO), cha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.
Kama alivyodai wakati anatoa ushahidi wake kwenye kesi hiyo ndogo, kuwa alimpokea Ling’wenya na mwenzake Adam Kasekwa, kwenye mahabusu ya kituo hiko, tarehe 7 Agosti 2020, ilihali washtakiwa hao wanakana hawakufikishwa na au kupokelewa na Msemwa, kituoni hapo.
Lakini mawakili wa jamhuri waliipinga barua hiyo wakidai kwamba shahidi na nyaraka hiyo vimekosa uwezo, huku hoja nyingine ikidai kuwa mshtakiwa huyo alishindwa kuonesha mlolongo wa utunzwaji wa kielelezo hicho hadi kumfikia (Chain of Custody).
Hoja nyingine ilidai barua hiyo siyo ya muhimu huku ya mwisho ikidai kwamba shahidi huyo wakati anatoa ushahidi wake hakujenga msingi wa kuitoa nyaraka hiyo mahakamani.
Mbali na Mbowe na Ling’wenya kwenye kesi hiyo, wengine ni Adam Kasekwa na Halfan Bwire ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kupanga njama za vitendo vya ugaidi maeneo mbalimbali nchini na kudhuru viongozi wa serikali.
Kwa sasa, Ling’wenya anaendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joachim Tiganga.