Afisa Msemaji wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema wameshtukia janja janja zinazopangwa na wapinzani wao juu ya wachezaji wao ili wakosekane kwenye mchezo ujao dhidi ya Simba Disemba 11.
Bumbuli amesema, "Tumebaini janja janja za wapinzani wetu kuwatafutia kadi za njano wachezaji wetu nyota au kufanyiwa rafu za makusudi akiwamo, Khalid Aucho na wengine ili kushindwa kucheza mechi ijayo dhidi ya Simba".
"Tumegundua na tunatarajia mechi yetu dhidi ya Mbeya Kwanza itakuwa na mabadiliko ya kikosi, baadhi ya nyota watapumzishwa kwa ajili ya kujiandaa na pambano letu dhidi ya Simba, tunawahakikishia mashabiki wetu tutarejea na pointi tatu kutoka kwa Mbeya Kwanza halafu Disemba 11 tabu iko pale pale dhidi ya Simba" Amesema Bumbuli.
Baada ya kusema hayo, Yanga inataraji kusafiri Jumapili ya kesho Novemba 28, 2021 kuelekea jijini Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.
"Msafara wetu utakuwa na nyota 22 na tunatarajia kuondoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya siku ya Jumapili kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza. Tunajua ni timu ambayo imejipanga pia na imeanza msimu vizuri"
Naye kocha wa Yanga Mohammed Nasreddine Nabi amesema, "Tumepata siku za kutosha kurekebisha mapungufu yote ambayo yalitupa changamoto, Lakini pia wapo wachezaji ambao tuliwakosa kutokana na maumivu na wakati huu tutakuwa nao"
Yanga ndiye kinara wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania wakiwa na alama 16 wakati Mbeya kwanza wapo nafasi ya 10 ikiwa na alama baada kila mmoja kucheza michezo 6.