BONDIA mstaafu raia wa Marekani, Mike Tyson ameteuliwa na Serikali ya Malawi kuwa balozi wa bangi nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)
Serikali ya Malawi kupitia ya Wizara ya Kilimo, imechukua hatua hiyo ikiwa ni miezi michache imepita tangu iidhinishe kilimo na matumizi ya bangi nchini humo tarehe 27 Februari 2020.
Tarehe 31 Agosti mwaka huohuo ilipitisha sheria ya udhibiti wa bangi ambayo itaanza kutumika mwaka 2022.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa tarehe 1 Novemba, 2021 na Waziri wa Kilimo, Lobin Clarke Lowe, Serikali ya nchi hiyo imemuomba Tyson maarufu kama ‘ Mike Iron’ kukubali ombi hilo ili kuisaidia nchi hiyo kushiriki kikamilifu katika kilimo cha bangi.
Waziri wa Kilimo, Lobin Clarke Lowe
“Baada ya Malawi kuhalalisha bangi, hatua hii imeibua fursa za kilimo halali cha bangi kwa madhumuni ya matumizi ya dawa, viwandani na kuipa nchi fursa ya kubadilishana uwezo wa uendezaji wa kilimo nchini pamoja na uwezekano wa kupata fedha za kigeni zinazohitajika.
“Licha ya manufaa yote yanayoonekana, Malawi haiwezi kumudu peke yake kutekeleza malengo ya kilimo hiki kwa ufanisi hasa ikizingatiwa ni sekta ngumu inayohitaji ushirikiano.
“Kwa hiyo ningependa kukuteua wewe Bw. Mike Tyson, kama Balozi wa Tawi la Bangi nchini Malawi. Tafadhali ukubali uteuzi huu,” aliandika Waziri huyo.
Katika siku za karibuni viongozi wa serikali ya Malawi akiwamo waziri huyo wa kilimo amekuwa akihamasisha wananchi wa Malawi kushiriki katika kilimo hicho cha bangi na kuunda vyama vya ushirika ili kupata zana za kilimo kwa urahisi.
Hadi kufikia Novemba mwaka huu, Serikali ya nchi hiyo ilikuwa imekwishatoa leseni za kilimo cha bangi kwa makampuni 72 ya ndani nan je ya nchi hiyo iliyo kusini mwa Afrika. Leseni moja hulipiwa ada ya Dola za Marekani 10,000 sawa na Sh milioni 22.
Sasa Malawi imeungana na nchi za Zimbabwe, Rwanda, Morocco na Lesotho Barani Afrika zilizoidhinisha bangi.
TYSON NA KILIMO CHA BANGI
Tyson ni mmoja wa mastaa wanaomiliki kampuni ya bangi huko katika jimbo la California nchini Marekani ambalo liliidhinisha matumizi ya bangi.
Kupitia kampuni hiyo inayofahamika kwa jina la Tyson Holistic Holdings Inc. aliyoianzisha mwaka 2016, bondia huyo anadaiwa kuingia kiasi cha Dola za Marekani 500,000 kwa mwezi sawa na (Sh bilioni 1.2).
Hata hivyo, Tyson ambaye alianza masumbwi ya kulipwa mwaka 1985 na kustaafu mwaka 2005, hivi karibuni ametangaza kufungua kampuni nyingine ya kilimo cha bangi inayofahamika kwa jina la Tyson 2.0. itakayosambaa sehemu mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa mtandao wa TMZ, Tyson ameungana na mastaa wengine wa Marekani kuwekeza kwenye kilimo cha bangi ambao ni ni Ray J, Whoopi Goldberg, Snoop Dogg, Rick Ross, Method Man & Redman, Wiz Khalifa na wengine ambao wamewekeza kisheria kwenye biashara za bidhaa za bangi.