WATU watano wilayani Lindi, wanadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na kupelekwa kusikofahamika nyakati za usiku wakiwa majumbani mwao wamelala.
Tukio hilo lililothibitishwa na polisi, viongozi wa vijiji husika na ndugu waliotekwa, linadaiwa kutekelezwa usiku wa Oktoba 30, mwaka huu na kundi la watu wenye silaha za moto.
Wanaodaiwa kutekwa ni Ismaili Uwesu Yahaya, Shazir Mohamedi Chileu, M’baraka Ally Maliki, Hamisi Said Liendeko, wakazi wa Kijiji cha Rutamba ya sasa na Mussa Fukutu wa Kijiji cha Michee.
Wakazi wa maeneo yaliyotokea tukio hilo, Husna Mohamedi, Esha Mohamedi na Husna Issa, wamedai kwamba kundi hilo lilikuwa limevalia nguo za kiraia likiwa na bunduki na kwenda kwenye nyumba za watu hao kisha kuvunja milango na kuingia ndani, huku wakiwaamuru waume zao kufungwa pingu.
Imedaiwa kuwa watu hao walifanya upekuzi na kuondoka na vitambulisho zikiwamo kadi za benki na wanawake wakiamriwa kuendelea kulala bila ya kupiga kelele.
“Usiku tukiwa tumelala usingizi tukasikia milango ya nyumba ikivunjwa, tulipoamka tukaamriwa tukae kimya,” alidai mmoja wa wanawake hao.
Pia walidai kitendo cha kutekwa kwa waume zao kinaendelea kuwapa wakati mgumu wa maisha, ikizingatiwa wana familia wakiwamo watoto wanaosoma.
Abdulrahman Bakari Awadhi, Mwenyekiti wa Serikali ya Vijiji vya Rutamba ya sasa na Michee, amekiri wananchi wao kutekwa na kudai mpaka sasa hawajafahamu eneo walikopelekwa, licha ya kupita kuulizia vituo mbalimbali vya polisi.
“Vituo vya polisi kwetu Rutamba na Wilaya Lindi mjini tumefika kuulizia tumeambiwa hawana taarifa yoyote kuhusu hilo,” alidai kiongozi huyo.
Alidai hilo ni tukio la pili kutokea mwaka huu, mwezi Januari 2021, watu wawili wanaume walitekwa na kupelekwa kusikojulikana na hawajarejea hadi leo.
Shaziri Mohamedi ni Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), alimwambia mwandishi wa taarifa hii kuwa waliokamatwa ni wanachama wa chama hicho na hafahamu sababu za kukamatwa kwao wala walikopelekwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Foka Dinya, alithibitisha ofisi yake kupokea taarifa hiyo, na kwamba wanaendelea kufuatilia ili kufahamu wanaohusika na matukio ya utekaji watu ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.