Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema kuna tishio la kutokea wimbi la nne la ugonjwa wa Uviko-19 kutokana na viashiria vitatu vilivyotajwa kuwa ni pamoja na ongezeko la visa vipya na aina mpya ya virusi katika baadhi ya nchi duniani.
Shirika la Afya Duniani jana liliripoti kuwa kuna aina mpya ya kirusi cha Uviko-19, kiitwacho Omicron, kinachosemekana kuwa na uwezo wa kusambaa haraka.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Novemba 27, 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale wakati akitoa tamko kuhusu hatua za kujikinga dhidi ya wimbi la nne la maambukizi ya ugonjwa wa huo.
Kiashiria kingine kilichotajwa ni pamoja na kuwepo kwa wasafiri wengi ndani na nje ya nchi katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na asilimia ndogo ya watu waliochanja nchini.
“Kutokana na hali hii hatuna budi kuendelea kuchukua hatua sahihi za kujikinga dhidi ya ugonjwa huu, Wizara inasisitiza kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga ikiwemo kuendelea kujitokeza kupata chanjo,” amesema.
Dk Sichwale amesema chanjo zimeonyesha ufanisi mkubwa dhidi ya madhara ya Uviko- 19. Amewataka wananchi kuendelea na uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi, kufanya mazoezi na kutumia tiba asili zinazoshauriwa na wataalamu.
Kuendelea kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kila sekta kuendelea kutekeleza miongozo ya kujikinga, kuimarisha uchunguzi wa wasafiri katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu na kufanya ufuatiliaji wa nchi zenye ongezeko la wagonjwa na kuchukua hatua stahiki.
Hadi Novemba 26 jumla ya wagonjwa 259,502,031 na vifo 5,183,003 vimetolewa taarifa Duniani.
Tangu ugonjwa huu uingie nchini Machi 16, 2020 jumla ya wagonjwa 26,261 na vifo 730 vilitolewa taarifa.
Kwa ujumla maambukizi yameanza kuongezeka duniani na baadhi ya nchi zina viashiria vya uwepo wa wimbi la nne la maambukizi ya ugonjwa huu.