Tukio lisilo la kawaida limetokea katika Barabara ya Interstate 5, San Diego katika Jimbo la California nchini Marekani ambapo mamilioni ya dola za Kimarekani yamemwagika barabarani na kusababisha taharuki kubwa, huku madereva wakipaki magari yao na kuanza kujizolea.
Video za tukio hilo, zilianza kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, mwanadada maarufu Demi Bagby akiwa wa kwanza kurekodi video akiwa eneo la tukio na kulipandisha kwenye akaunti yake ya Tik Tok ambapo ndani ya muda mfupi ilisambaa kwa kasi na kuwaacha watu wengi wakiwa na mshangao.
Taarifa za awali zilieleza kwamba mtu ambaye hakufahamika, akiwa ndani ya gari lake ambalo namba zake za usajili zilikuwa zimefunikwa kwa taulo, ndiye aliyemwaga fedha hizo barabarani ili watu wajiokotee.
Hata hivyo, haukupita muda mrefu kabla ya mamlaka husika kutoa tamko ambapo Polisi wa Usalama Barabarani jimboni California, CHP, kupitia kwa msemaji wake, Sajenti Curtis Martin walieleza kuwa tukio hilo limetokea Ijumaa ya Novemba 19, 2021 katika eneo la Carlsbad, San Diego majira ya saa tatu na robo asubuhi. #dola #demibagby