No title



Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeahirisha usikilizaji wa kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, kutokana na shahidi wa sita wa Jamhuri kutohudhuria mahakamani hapo, kwa sababu za kiafya. .

Kesi hiyo imeahirishwa leo Jumatano, tarehe 3 Novemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joackim Tiganga, baada ya upande wa jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, kuomba ahirisho.
 
Wakili Kidando ameieleza mahakama hiyo kuwa, shahidi huyo ambaye alitarajiwa kuwa wa sita kati ya 24 ambao upande wa mashtaka umepanga kuwaita, amepata ugonjwa hivyo ameshindwa kufika mahakamani.

“Mheshimiwa Jaji tumempata shahidi tuliyepanga kuendelea naye leo lakini amepata tatizo la kiafya, amepata ugonjwa na kushindwa kuja mahakamani. Kwa sababu hiyo tunaomba ahirisho la kuleta shahidi mwingine kesho,” amesema Wakili Kidando.

Baada ya maombi hayo, Jaji Tiganga amewauliza upande wa utetezi ambapo kiongozi wa japo la mawakili, Peter Kibatala amesema hawana pingamizi.

Mara baada ya Kibatala kueleza hayo, Jaji Tiganga ameiahirisha kesi hiyo hadi kesho Alhamisi saa 3:00 asubuhi na watuhumiwa wataendelea kuwa mahabusu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad