Mahakama nchini Kenya inatarajiwa kutoa uamuzi wake iwapo maafisa wanne wa polisi wana hatia ya mauaji ya Alexander Monson, raia wa Uingereza, ambaye alipatikana amefariki karibu miaka 10 iliyopita akiwa mikononi mwa polisi katika mji wa pwani wa Diani.
Maafisa hao wa polisi walifikishwa mahakamani mapema mwaka huu, baada ya kubainika kuwa Bw Monson alifariki baada ya kupigwa akiwa kizuizini na wala si kutokana na kutumia dawa za kulevya kupita kiasi kama polisi walivyodai awali.
Bw Monson, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 28, alikuwa mwana wa 12 wa Baron Monson na mrithi wa mali ya familia huko Lincolnshire, na alikuwa akiishi na mamake huko Diani, Kenya alipofariki.
Baba yake, Lord Nicholas Monson, mtu wa tabaka la juu nchini Uingereza, ambaye aliwasili Kenya wikendi iliyopita atahudhuria uamuzi wa mahakama.
Bw Monson alikamatwa kwa madai ya kuvuta bangi na licha ya polisi kusema alikufa kutokana na matumizi ya kupita kiasi, ripoti za uchunguzi wa sumu zilionyesha kuwa hakuna dawa zilizopatikana katika mfumo wake wakati wa kifo chake.