MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru aliyekuwa mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake wawili baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka washtakiwa hao walitenda makosa yaliyokuwa yanawakabili
Gugai na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 43 kati ya hayo yapo ya kughushi, utakatishaji fedha kumiliki mali ambazo hazina maelezo zenye thamani ya sh. Bilioni 3.6
Hukumu hiyo imesomwa leo Novemba 12,22021 na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba. Mbali na Gugai, wengine ambao wameachiwa ni George Makaranga na Leonard Aloys
Akisoma hukumu hiyo Simba amesema, ameyaweka mashtaka hayo 43 yanayowakabili washtakiwa katika makundi matatu moja likiwa ni la kujipatia mali zisizoelzeka,kughushi na kujipatia fedha zaidi ya kipato chake.
Amesema amepitia ushahidi wa mashahidi 42 wa upande wa mashtaka waliopelekwa kudhibitisha mashtaka ya kughushi lakini wameshindwa kudhibitisha.
Amesema katika shtaka la kujipatia mali zisizoelezeka, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha uhalali wa umiliki wa mali hiyo inayomilikiwa na Gugai huku pia katika shtaka la kughushi Simba amesema mahakama imethibitisha kuwa uuzwaji wa nyumba hizo zilizokuwa zikimilikiwa na Gugai ni halali na sio kughushi kwani lilifanyika mbele ya wakili Beatus Malima.
Amesema, upande wa mashtaka kama wangetaka wangepata nafasi ya kumleta wakili huyo ilinkuthibitisha na kama si kweli basi angeshtakiwa.
"Ikiwa mashtaka ya ubadhirifu wa mali na kughushi nyaraka yameshindwa kuthibitisha na hayana uwezo wa kuwatia hatiani washtakiwa hao hata mashitaka ya kujipatia fedha nje ya uwezo wake na yenyewe kukosa uwezo wa kuwatia hatiani washtakiwa moja kwa moja, hivyo mahakama inawaachia huru washtakiwa wote.
Baada ya kusema hivyo mshtakiwa Gugai alipiga ishara ya msalaba ishara ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuinua mikono juu na wenzake.
Nje ya Mahakama, Wakili wa utetezi, Alex Mgongorwa, amedai kuwa hukumu hiyo imezingatia Sheria, hivyo wameridhika na uamuzi huo
Katika kesi hiyo, Gugai na wenzake walikuwa wanakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.