Majaliwa akerwa wanaume kukacha kupima Ukimwi




Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya tabia ya wanaume ya kuwatumia wake zao kwenda kwenye vipimo vya maambukizi ya virusi vya Ukimwi huku wao wakikataa kwenda kupima.


Majaliwa amesema leo Ijumaa Novemba 26, 2021 mkoani Mbeya wakati akifungua kongamano la kisayansi katika wiki ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa inafanyika jijini Mbeya.



Amesema kuwa tafiti zinaonyesha nchini wanaume hawana mamko wa kujitokeza kupima afya zao na badala yake wamekuwa wakitumia majibu ya wenza wao jambo ambalo sio sahihi.



''Jamani msiwe washawishi kwa wenza wenu kupima na wanaporejea majumbani unaulizia vipi vipimo, sasa ili tuwe salama lazima tukapime afya na ikibainika kuna maambukizi waanze kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi ili kuweza kupanga mipango endelevu kwa maslai mapana ya Taifa ''amesema.



Majaliwa amesema kuwa mipango mizuri katika familia inatokana  na afya bora ni vyema  wanaume kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kujitokeza kupima maambukizi ya VVU na hata kuchanja ugonjwa wa Uviko-19  ili kuwa salama na kuunga mkono juhudi za Serikali na mipango endelelevu kwa mustakabali wa Taifa.



Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuthibiti Ukimwi (Taciads), Dk Leonard Maboko amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kutafakari kwa kina tafiti na kufikia malengo ya dunia kuteketeza maambukizi ya virusi vya ukimwi na kufikia asilimia 0 kwa vifo ifikapo 2030.



Dk Makobo amesema mwaka 2016/17 wamebaini kiwango cha wanaume kupima VVU kilikuwa chini na ndio sababu ya kuomba Waziri Mkuu kuwa balozi jambo ambalo limeleta hamasa kwa wanaume kuanza kupima.



''Waziri Mkuu asilimia 40 ya vijana wenye umri wa miaka 15 wamepata maambukizi na hayo yote yametokana na tafiti mbalimbali zinazofanywa kwa kushirikiana na wadau''amesema.



Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kuwa Mkoa wa Mbeya ni kinara kwa maambukizi kwa kuwa na asilimia 9.3 na hivyo kama wabunge wamekubaliana kukabiliana na janga hilo na kuwezesha kufikia asilimia 0 ifikapo 2030



''Waziri Mkuu licha ya Mkoa wa Mbeya  kuwa  kinara kwa maambukizi lakini ikumbukwe wakati wa takwimu hizo zikitolewa ilikuwa ni mkoa mmoja  na sasa iligawanyishwa na Mkoa wa Songwe tunasubiri tafiti za  mgawanyo wa takwimu za mwaka 2022 utakaofanywa na Taciads. '' amesema.



Naye Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Godwin Molle amesema kuwa tayari wamepokea Sh6.1 Bilioni kutoka Serikali kwa ajili ya tafiti ya tiba ya Sayansi jambo ambalo litaleta matokeo mazuri katika Wizara ya Afya.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad