WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana matumaini makubwa na Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars) na anaamini itafanya vizuri na kufuzu kushiriki kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar 2022.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 5, 2021) wakati alipozungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania, (Taifa Stars) katika Hoteli ya Golden Tulip, Jijini Dar es Salaam ambapo timu hiyo imeweka kambi ili kujiandaa na michezo ya awali ya kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Timu ya Taifa ya DR Congo na Madagascar.
Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Michezo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wataendelea kuisimamia na kufuatilia maendeleo ya timu hiyo ya Taifa hadi hatua ya mwisho na kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.
“Rais ana matumaini makubwa na nyinyi na anawatakia kila la kheri katika maandalizi yenu, Ni matumaini yake kuwa mtafanya vyema na kufuzu hatua ya kumi bora na hatimaye kupata nafasi kuwa miongoni mwa timu tano zitakazo shiriki kombe la Dunia kutoka Afrika.
Waziri Mkuu amewasihi wachezaji wa timu ya Taifa kujitoa na kufanya mazoezi kwa bidii, pamoja na kuzingatia maelekezo wa Mwalimu na wataalam wa benchi la ufundi ili kuhakikisha Ushindi unapatikana.
“Viongozi wa kamati ya Hamasa ya Taifa Stars kwa Kushirikiana na TFF hakikisheni mnaisimamia timu vyema, Wachezaji wale vizuri na wafanye mazoezi na wapewe kila kinachohitajika ili kujihakikishia tunapata ushindi.”
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha wa Taifa Stars John Bocco ameahidi kuwa watajitoa kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi zote zilizobaki.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi kutoka TFF wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Wilfred Kidau, Viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania BMT, Mwenyekiti wa kamati ya Hamasa ya Taifa Stars, Ghalib Mohamed na Makamu Mwenyekiti Salim Abdala “Try Again” na Katibu wa Kamati hiyo Hersi Said.