Je wewe ni mtu wa kupenda ghafla, yaani mwanaume anapokutamkia kwamba anakupenda huwa unamuamini kwa kiasi gani, unakuwa ni mwepesi wa kumuamini na kujitoa kwa ajili yake au unakuwa na kujivuta vuta ili kujiridhisha kabla ya kuingia katika uhusiano? Hebu fikiri kabla ya kuamua, jipe muda kwani hakuna jambo lililo jema kama subira linapokuja swala la kupenda. Subira itakuepusha kupoteza muda wako katika mahusiano ambayo hayana mashiko wakati dhamira yako ilikuwa ni kumpata mwenzi mwenye sifa muafaka, pale utakapoingia mahali ambapo sipo. Kwa kawaida kutoka katika uhusiano huo kuna gharama kubwa na kunaweza kukusababishia matatizo mengi yakiwemo ya kiafya.
Hapa chini nitajaribu kueleza makosa kadhaa ambayo wanayafanya wanawake linapokuja swal la kupenda:
1.Kumbadili mtu awe vile utakavyo:
Usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha mtu mzima na akili zake. Kama umepata mwanaume ambaye kwa mtazamo wako unamuona ana sifa muafaka lakini anatabia ambazo huzipendi kwa mfano ulevi au kuvuta sigara vitu ambavyo vinakukera sana, usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha na akaacha tabia hizo, anaweza kuacha kwa muda tu ili kukuvuta ukiingia kingi imekula kwako, tabia hiyo inaweza kujirudia. Ni vyema kama kuna tabia ambazo umezipenda lakini zipo ambazo huzipendi kutoka kwa mwenzi wako, basi weka uzingativu kwenye zile tabia unazozipendfa na zile usizozipenda achana nazo, kama ataamua mwenyewe kuziacha sawa lakini kama akiamua kuendelea nazo, basi zisikuumize kwani unaweza kujikuta ndoa yako inakuwa na migogoro isiyokwisha kwa sababu ya kuonekana una ghubu kwa kujaribu kumbadilisha mwenzi wako na mwisho wake upendo unakuwa haupo na kisirani katika ndoa kinaongezeka. Kitendo cha kuonekana kuwa na ghubu kinaweza kumuingiza mwanaume katika tabia nyingine mbaya ya kutotumia muda mwingi kukaa nyumbani kwake na kutafuta kampani nyingine, kama akipata kampani ambayo siyo nzuri anaweza kuangikia katika nyumba ndogo ambayo itamkubali bila masharti.
2.Njoo tuishi:
Unaweza kukutana na mwanaume ambaye ana nyumba nzuri au amepanga nyumba nzuri na ana kila kitu ndani pamoja na usafiri, anakuwa mwepesi kukupa funguo za nyumba yake ili uhamie muishi pamoja, lakini haweki msimamo wake wazi kwamba ana matarajio gani na wewe. Kabla ya kukubali kupokea funguo na kuhamia kwake jiulize kama unampenda kwa dhati au umekubali kwa sababu ya nyumba yake nzuri. Kumbuka nyumba na vitu vingine vinavyotizamika kwa macho (material things) havina mashiko linapokuja swala la kupenda. Kupenda kunahusisha vitu vya ndani kama vile kupenda kwa dhati bila masharti wala kuangalia sifa za nje, kuwa na amani moyoni kila umwonapo mpenzi wako, kuwa na furaha wakati wote mnapokuwa pamoja, kupatwa na msisimko wa mapenzi kila umwonapo au usikiapo sauti yake nk. Lakini kama utamkubali mwanaume kirahisi kwa sababu tu kakukabidhi funguo za nyumba yake wakati huna mapenzi ya dhati ni janga kubwa kwa sababu hivi vitu vya nje vinaweza kutoweka kirahisi, sasa je ikitokea si mapenzi nayo yatakuwa yamekwisha? Kumbuka kwamba kile kilichokupeleka kwake hakipo.